Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AIPONGEZA WIZARA KUIPELEKA TIMU YA WENYE ULEMAVU KOMBE LA DUNIA


**********************
Na. John Mapepele

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuitunza na kuijengea mazingira mazuri timu ya Taifa ya Soka ya wenye ulemavu (Tembo Warriors) iliyofuzu kucheza kombe la dunia mwakani Oktoba 2022 nchini Uturuki ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Mhe. Rais ameyasema haya leo Disemba 7, 2021 Ikulu ya Dar es Salaam kwenye hafla maalum aliyoialika timu ya Tembo, kufuatia kufanya vizuri katika mashindano ya soka ya Afrika ya wenye ulemavu (CANAF 2021) yaliyoisha hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Tembo Warriors kufuzu kuingia kwenye kombe la dunia baada ya kushika nafasi ya nne.

“Niwapongeze watoto wangu mmekonga nyoyo na mmetoa somo kwamba mnaweza pia mmeandika historia” amesisitiza Mhe. Rais Samia.

Rais Samia ameishukuru na kuipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo na wageni kutoka kwenye mataifa mbalimbali kurejea kwao salama.

Akizungumzia kuhusu ombi la Wizara la kuitaka kurejea bajeti kwa ajili ya gharama ya kuzisaidia timu za taifa zinazofanya vizuri, amesisitiza kuwa suala hilo amelibeba ili kuona jinsi ya kulishughulikia.

“Tunajua umuhimu wa fedha, Serikali tunalibeba na kuona jinsi ya kulifanyia kazi ". Amesisitiza Mhe.Rais

Ameielekeza, Wizara kuangalia namna bora ya kuiandaa timu mahali pamoja ili iweze kufanya maandalizi ya muhimu badala ya kuwaacha wachezaji watawanyike hali ambayo itawafanya washindwe kujiandaa vema kuelekea kombe la dunia.

Aidha, amewataka wachezaji wa timu hiyo kuwa makini na kuendelea kucheza kwa bidii ikizingatiwa kuwa mashindano yanayofuata yatachezewa nje ya nchi.

Kuhusu ombi la Shirikisho la Soka kwa wenye ulemavu la kumwomba awe mleze wa timu hiyo amesema atawatafutia mtu atakayewafaa kwa kuwa yeye ana makujumu mengi ya kitaifa.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema, Serikali itaendelea kusimamia timu za Taifa za michezo zinazofanya vizuri na kufika katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bahungwa amemshukuru Rais kwa kuihamasisha na kuisaidia timu hiyo ambapo alitoa shilingi milioni 150 kusaidia maandalizi ya mashindano hayo ili timu hiyo ishinde kupitia kwa Mhe. Waziri Mkuu.

Rais wa Shirikisho la Soka kwa wenye ulemavu nchini, Peter Sarungi amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake uliotukuka ambapo amesema amekuwa akiongoza kwa upendo bila kubagua na kutushirikisha watu wenye ulemavu.

Akiwatambulisha wageni waliohudhulia katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema timu hiyo ilipambana vikali na kuzitoa timu za mataifa mbalimbali ambapo amemtambulisha kwa Mhe. Rais mshambuliaji wa timu hiyo Frank Ngailo kuwa ndiye mchezaji bora wa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments