Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MHAGAMA AWATAKA WENYE VIWANDA KUIMARISHA AFYA, USALAMA NA MASLAHI YA WAFANYAKAZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na wawekezeshaji wa kiwanda cha Kioo Limited kilichopo Wilayani Temeke Mkoani Dar es salaam alipofanya ziara akiambatana na baadhi ya Viongozi wa OSHA kwa lengo la kukagua mifumo ya usalama na afya na kuangalia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (SBAU), Mhe.Jenista Mhagama (Mb),(wapili kushoto) akitoa maelekezo kwa viongozi wa kiwanda cha kuzalisha Mabati cha Alaf Limited alipofanya ziara katika kiwanda hicho kwa lengo la kuangalia uzingatiaji wa kanuni za Usalama na Afya ya mahali pa kazi pamoja na masuala mengine ya kazi. Aliokaa nao meza kuu ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (Wakwanza kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Alaf Limited, Ashish Mistry (watatu kushoto) na Meneja Uhusiano wa Alaf Limited, Bi. Hawa Bayumi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (SBAU) Mhe.Jenista Mhagama (Mb), akiwa katika kikao na viongozi wa OSHA Kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu kabla ya kutembelea kiwanda kinachozalisha mabati cha Alaf Limited pamoja na kiwanda cha Kioo Limited vilivyopo Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya kwa wafanyakazi pamoja na ustawi wa wafanyakazi ikiwemo maslahi yao.


Baadhi ya Viongozi wa Kiwanda cha Alaf Limited wakiwa katika kikao cha tathmini fupi ya kiwanda hicho tangu kuanzishwa kwake, wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi OWM (SBAU) Mhe.Jenista Mhagama (Mb) ambapo aliambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda pamoja na baadhi ya watendaji wa OSHA.

***************************

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ametoa wito kwa wenye viwanda nchini kuimarisha mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi ili kuleta tija katika uzalishaji na ukuaji wa biashara zao.

Ametoa wito huo alipofanya ziara katika kiwanda cha Alaf Limited kinachozalisha mabati na bidhaa nyinginezo za chuma pamoja na kiwanda cha Kioo Limited kinachozalisha bidhaa mbalimbali za vioo. Viwanda hivyo vipo Manispaa ya Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika maelezo yake ya awali kwa menejimenti za viwanda husika, Waziri Mhagama alieleza kwamba dhumuni la ziara yake ilikuwa ni kuangalia jinsi viwanda hivyo vinavyozingatia masuala ya Usalama na Afya kwa wafanyakazi pamoja na masuala mengine yanayohusu kazi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.



“Kama walivyoeleza katika taarifa yao, kiwanda hiki kina miaka 61 tangu kilipoanzishwa na serikali yetu ni mbia wa kiwanda hiki hivyo tunapoadhimisha miaka 60 ya Uhuru tumeona ni vema tukatembelea kiwanda hiki ili tuweze kuona katika kipindi hicho chote kiwanda kimepata mafanikio gani?,” alisema Mhagama na kuongeza:



“Kupitia taarifa iliyowasilishwa na viongozi pamoja na yale niliyoyaona nilipotembelea maeneo tofauti katika viwanda hivi nimefarijika kuona wamefanikiwa katika mambo mengi ikiwemo kuimarisha mifumo ya usalama na afya kwa wafanyakazi, maslahi ya wafanyakazi yameendelea kuboreshwa kupitia uwepo wa mikataba ya hali bora. Aidha, nimeona kiwango cha kodi mnachochangia kwenye mapato na mfuko mkuu wa serikali ni kikubwa ambapo kwa upande wa Alaf Limited kwa miaka mitano iliyopita kiwanda kimechangia zaidi ya bilioni 290 kiwango ambacho kinaridhisha.”



Katika ziara hiyo, viongozi wa viwanda vyote viwili walipata fursa ya kuwasilisha taarifa fupi kuhusu utendaji wao, mafanikio pamoja na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika uzalishaji ambapo miongoni mwa mafanikio yaliyoelezwa ni pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 500 kwa kila kiwanda pamoja na kuchangia kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.



Katika ziara hiyo Waziri Mhagama aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda pamoja na watendaji wengine wa OSHA ambapo Bi. Mwenda amewapongeza viongozi wa viwanda vya Alaf Limited na Kioo Limited kwa kushirikiana vema na Taasisi yake katika kuweka mifumo madhubuti ya kulinda nguvukazi suala ambalo ndilo jukumu la msingi la OSHA.



“Kwakweli wote mliojumuika nasi katika ziara hii mmejionea jinsi viwanda hivi vilivyoweka mifumo mizuri ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi hivyo nawapongeza sana wenye viwanda hivi kwa kushirikiana nasi katika kutimiza wajibu wetu wa kuwalinda wafanyakazi pamoja na kulinda mitaji ya wawekezaji dhidi ya majanga mbalimbali. Aidha, nawaahidi tu kwamba tutaendelea kushirikiana nao kwani jukumu letu ni kuwawezesha wawekezaji na sio kuwakwamisha katika shughuli zao za uzalishaji,” alieleza Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.



“Alaf ni kampuni kubwa ambayo ina miaka 61 sasa na tunatarajia itaendelea kukua zaidi hadi kufikia miaka 120 na zaidi na pia napenda kusema kwamba tumefarijika sana kupokea ugeni huu kwa siku ya leo na tunamshukuru sana Mhe. Waziri Mhagama kwa kututembelea ili kujua mafanikio na changamoto zetu na hivyo kutusaidia kuzitatua,” amesema Ashish Mistry, Mkurugenzi Mkuu wa Alaf Limited.



Kwa upande wa Meneja Rasilimali Watu wa Kioo Limited, Bw. Jacob Msuya, ameishukuru OSHA kwa kuwapa miongozi ya mara kwa mara kuhusu uzingatiaji wa viwango vya usalama na afya mahali pa kazi hususan kupitia mfumo mpya wa kieletroniki wa Usimamizi wa Maeneo ya Kazi ujulikanao kama WIMS yaani Workplace Information Management System ambao alieleza kwamba umeondoa urasimu wa huduma za OSHA.

Post a Comment

0 Comments