Ticker

6/recent/ticker-posts

BALOZI MULAMULA APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO UNHCR, UNFPA

Na Mwandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bibi. Mahoua Parums pamoja na Mwakilishi Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) Bw. Mark Bryan Schreiner katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amewaeleza Bibi. Parums na Bw. Schreiner kuwa UNHCR na UNFPA zimekuwa na mchango mkubwa kwa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kushughulikia masuala ya wakimbizi pamoja na kukuza maendeleo.

“Tumekubaliana na UNHCR kuendelea kushirikiana kwa karibu pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani katika mchakato wa kurudisha wakimbizi wa Burundi nchini kwao kusudi hali ya Burundi iendelee kutengamaa kwani kurudi kwa wakimbizi hao kutachangia maendeleo ya Burundi,” amesema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa itakumbukwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye alipofanya ziara ya kitaifa hapa nchini Oktoba 2021 alitoa rai ya wakimbizi wa Burundi warudi nchini kwao ili kuweza kuchangia maendeleo ya Taifa hilo.

Pia Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mwakilishwa wa UNFPA amekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatarajia kuanza zoezi la Sensa mwezi Augusti 2022 na hivyo kutoa rai kwa Shirika hilo kuwashirikisha na kuwawezesha vijana na wanawake wa kitanzania katika maendeleo ya teknolojia.

“Rai yangu kwao ni kuwahusisha vijana na wanaweke kwani UNFPA mbali na kushughulika na idadi ya watu wana program ya kuwashirikisha na kuwawezesha vijana ni vyema washirikiane kwa pamoja na Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kwa maendeleo ya pande zote mbili,” Amesema Balozi Mulamula.

Kwa upande wake Mwakilishi wa UNHCR Bibi. Parums ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapokea na kuwalinda wakimbizi kwa muda mrefu.

“Tumekubaliana kushirikiana kwa pamoja na Serikali katika kuwalinda na kuwasaidia wakimbizi na kuwapatia baadhi ya mahitaji muhimu……tunaomba tuendeleze ushirikiano huu kwa maendeleo yetu,” amesema Bibi. Mahoua.

Nae Mwakilishi wa UNFPA, Bw. Schreiner amesema UNFPA itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa inasonga mbele kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia katika zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Augosti 2022 ili kuiwezesha Tanzania kupata takwimu sahihi kuhusu idadi ya watu na kuiwezesha kusonga mbele kimaendeleo.

Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bibi. Sarah Gordon-Gibson.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na WFP.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bibi. Mahoua Parums katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mwakilishi Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) Bw. Mark Bryan Schreiner katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa UNHCR, Bibi. Mahoua Parums akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula.
Kikao baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Mwakilishi wa UNHCR, Bibi. Mahoua Parums kikiendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimueleza jambo Mwakilishi wa UNFPA Bw. Mark Bryan Schreiner katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa UNFPA Bw. Mark Bryan Schreiner akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bibi. Sarah Gordon-Gibson


Post a Comment

0 Comments