Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DK.MPANGO KUZINDUA SERA YA TAIFA YA MAZINGIRA



Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 5,2022 kuhusu Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 unaotarajiwa kufanyika Februari 12, 2022 Jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 unaotarajiwa kufanyika Februari 12, 2022 Jijini Dodoma. Wengine kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Bw. Edward Nyamanga, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) na Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba.

..................................................................

Na.Alex Sonna,DODOMA

Makamu wa Rais Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 inayotarijiwa kuzinduliwa 12 Februari, 2022 Jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Februari 5,2022 Jijini Dodoma ,Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga amesema Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 imejumuisha masuala ya mazingira yaliyokuwemo katika Sera ya 1997 na masuala mapya.

Ameyataja masuala mapya katika Sera mpya ya mwaka 2021 ni pamoja na: Udhibiti wa taka za kielektroniki, Usimamizi na matumizi ya kemikali, na Udhibiti wa uchafuzi katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.

Bi.Maganga amesema kuwa masuala mengine ni pamoja na Mabadiliko ya tabianchi; Usimamizi wa matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa; na Udhibiti wa viumbe vamizi.

“Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 imeongeza wigo wa masuala na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika ili kuleta maendeleo endelevu na imezingatia changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani” ameeleza Bi.Maganga.

Amesema kuwa, Serikali imeamua kuwa na Wiki ya Uzinduzi wa Sera itakayoanza tarehe 07-12/02/2022 ambayo itaambatana na shughuli mbalimbali za hifadhi ya mazingira ikiwa ni sehemu ya masuala ya msingi yanayoelekezwa katika Sera mpya.

Bi. Maganga amezitaja shughuli zitakazofanyika katika wiki hiyo kuwa ni Upandaji miti Jijini Dodoma katika maeneo ya Medeli, Iyumbu, Iseni na maeneo ya barabara inayoanzia Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuelekea barabara ya Dodoma Dar es Salaam.

Aidha,amesema kuwa watanya usafi pembezoni mwa barabara inayoanzia Shule ya Martin Luther hadi Wajenzi kupitia Nzuguni, Ilazo, Ipagala na Area C; Kutoa elimu kuhusu utenganishaji wa taka, kufanya Usafi katika soko la Changombe pamoja na Utoaji wa Elimu ya Mazingira kwa wananchi na wadau kupita vyombo vya habari.

Dhumuni la kuwepo kwa shughuli hizo ni kurejesha hali ya asili ya mazingira iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu kwa kuwa na zoezi la upandaji miti, kuboresha afya ya jamii na elimu ya utenganishaji taka kwa ajili ya udhibiti wa taka ngumu na kuwezesha urejelezaji wa taka kwenye bidhaa na huduma mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments