Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY ATAKA WATUMISHI WA AFYA KUBADILI FIKRA KATIKA UTENDAJI WA KAZI

Waziri wa Afya mhe. Ummy Mwalimu akiongea na wajumbe wa baraza la wafanyakazi kutoka Wizara Makao Makuu,Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vyuo vya Kitaaluma na Taasisi zilizo chini ya Wizara kwenye Mkutano wa baraza kuu la wafanyakazi unaofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa wizara ya afya Prof. Abel Makubi akiongea na wajumbe wa baraza hilo(hawapo pichani) wakati wa baraza la wafanyakazi ambapo amesisitiza kufanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya wizara.

Baadhi ya wajumbe kutoka kwenye hospitali za Rufaa za Mikoa wakifuatilia hotuba ya waziri wa afya(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Baadhi wa wajumbe kutoka Wizara ya afya Makao Makuu akifuatilia kwa makini ufunguzi wa mkutano huo ambapo Waziri Ummy Mwalimu aliwataka kuhakikisha wanafanya kazi kama timu moja ili kupata matarajio ya pamoja katika kuwahudumia wananchi.

Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara ya afya Bi. Mary Ntira akisoma muhtasari wa kikao kilichopita kwenye Mkutano wa baraza kuu la wafanyakazi linalofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.


**********************


Na. Catherine Sungura na Emmanuel Malegi,WAF – Dodoma



Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watumishi wa umma katika sekta ya afya kubadili fikra za utendaji kazi na kuwa wabunifu katika kutatua changamoto ili kuongeza chachu ya kufikia malengo na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akifungua mkutano wa baraza kuu la wafanyakazi wa Wizara ya afya,hospitali za rufaa za mikoa pamoja na taasisi zilizo chini yake uliofanyika jijini Dodoma.

“Nitoe rai kwa watumishi wote kubadili fikra zetu katika utendaji na tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii tukilenga kufikia malengo na mafanikio tuliyojiwekea. Kila mmoja katika nafasi yake awe mbunifu katika kutatua changamoto zinazomkabili na hatimaye kutoa huduma bora”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani ametoa Shilingi bilioni 891.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu pamoja na huduma za afya hivyo amewataka watumishi watumie fursa zinazopatikana zikawe chachu za kupata mafanikio makubwa Zaidi.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja, Waziri Ummy ametaja kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa wajawazito wanaohudhuria kniniki kwa mahudhurio manne na Zaidi, kuimarisha na kuboresha na kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma katika Hospitali za rufaa za mikoa.

Kwa upande wa mahusiano na wawekezaji na sekta binafsi, Waziri Ummy amesema sekta binafsi zimesaidia kujenga viwanda vya kuzalisha dawa kupitia makubaliano ya pamoja na wawakilishi wa nchi, mashirika ya kimataifa pamoja na taasisi mbalimbali.

Aidha, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa ya milipuko ikiwemo UVIKO-19 kwa kuongeza vipimo vya haraka (Rapid Test) na nija ya vinasaba (RT-PCR). kuimarisha ubora wa takwimu za mifumo kielektroniki ya ugavi wa vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ngazi zote. Kuboreshwa kwa huduma za maabara na kupata ithibati ya kimataifa.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy ameeleza changamoto ambazo bado zinaikabili sekta ya afya ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi hasa wa kipato cha chini, upungufu mkubwa wa watumishi wanaohitajika katika vituo vya afya, upatikanaji wa huduma za dawa, uchakavu wa miundombinu, ufinyu wa bajeti pamoja na kuondelea kuongezeka magonjwa yasiyoambukiza.

Waziri Ummy amesema changamoto hizo zitatatuliwa endapo watumishi watakuwa na ari ya utendaji wenye matokeo, uzalendo, uadilifu na ubunifu Zaidi ili kuweza kukabiliana nazo.

Post a Comment

0 Comments