Ticker

6/recent/ticker-posts

DCPC YAADHIMISHA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI


Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Mkoa Dar es Salaam (DCPC) Chalila Kibuda akiongoza mkutano mkuu maalum wa wanachama DCPC uliofanyika katika Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam.
Wanachama DCPCkatika mkutano mkuu maalum.

***************

UMOJA Wa Klabu ya waandishi wa habari Tanzania (UTPC,) kwa kushirikiana na Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC,) wameadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa waandishi DCPC kupewa mafunzo maalum ya hali ya ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari pamoja na mchango wa UTPC katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo jijini Dar es Salaam leo Mei 9 2022, Afisa Programu wa UTPC Victor Maleko amesema, wamekuwa wakitengeneza mazingira bora ya usalama kwa wanachama katika kufanya kazi zao kwa kuhakikisha wanakuwa salama.

"UTPC tupo makini katika kuhakikisha waandishi wanakuwa sala wakati wakitekeleza majukumu yao, kuna miongozo na tunashirikiana na Serikali katika kufanikisha hilo." Amesema.

Pia ameishauri klabu hiyo kushirikiana katika kutatua changamoto kwa kuwashirikisha wanachama wake.

Awali akizungumza katika mkutano mkuu Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo amesema UTPC ipo tayari muda wowote katika kushirikiana na wanachama wake ili kuleta matokeo chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema DCPC inatakiwa kuwa kichwa katika utendaji kutokana na fursa kubwa zinazowazunguka, na kueleza kuwa katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari klabu 28 kote nchini zitaadhimisha siku hiyo kati ya tarehe 9 na 16 na UTPC imetoa fungu la kuendesha maadhimisho hayo.

Aidha amezielekeza klabu kutoa mrejesho wa fedha zinazotolewa na wafadhili ambao ni SIDA ili waweze kuona matumizi ya fedha hizo na kuweza kuendelea kudhamini.

Ameeleza kuwa utatuzi wa matatizo ni muhimu katika kujenga klabu imara yenye umoja na ushirikiano.

Kwa upande wake aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa DCPC Chalila Kibuda ameishukuru UTPC kwa kushiriki katika maadhimisho hayo na kuahidi ushirikiano katika kuendeleza gurudumu la habari kwa kuzingatia weledi wa kiwango cha juu.

Mkutano huo umekwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC.)

Katika Mkutano huo Maalum wa Chama cha Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC) umechagua viongozi wapya Sam Kamalamo (Mwenyekiti), Salome Gergory (Makamu Mwenyekiti), Fatuma Jalala (Katibu Mkuu), Chalila Kibuda (katibu Msaidizi) na Patricia Kimelemeta (Mweka hazina). Ni baada ya kuwaondoa waliokuwepo.

Wajumbe ni Ibrahimu Yamola, Tausi Mbowe, Salehe Mohamed, Janeth Josia, Njumai Ngota na Shaaban Matutu.

Post a Comment

0 Comments