Ticker

6/recent/ticker-posts

HUISHENI TAARIFA MUHIMU ZA MASHAURI: JAJI MKUU

Na. Faustine Kapama, Mahakama, Tanga.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kote nchini siku 14 kuhuisha taarifa muhimu za mashauri kwenye Mfumo wa Kuratibu Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS-II) ili kutekeleza azma ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao (e-Judiciary).

Mhe. Prof. Juma ametoa agizo hilo leo tarehe 17 Mei, 2022 katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga, ambapo amekutana na Wakuu wa Wilaya za Kilindi na Handeni, kukagua ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Kilindi na kuongea na watumishi katika Wilaya hizo mbili.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kilindi, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa amepata taarifa kuwa Mkoa wa Tanga unafanya vizuri kwenye eneo la kuhuisha taarifa kwenye JSDS-II, lakini kwa bahati mbaya, Mahakama Kuu zingine zimeanza kushuka na kurudi kwenye karne ya 19. Amezitaja Mahakama Kuu zinazofanya vizuri kuwa ni Tanga, Tabora, Mwanza, Musoma, Songea na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke.

“Mwishoni mwa mwezi huu wote tuingie kwenye ligi moja ya Tanga, Tabora, Mwanza, Musoma, Songea na Kituo Jumushi Temeke. Hawa wote ndiyo wapo kwenye mstari, wengine wote wameshaanza kubaki nyuma. Sasa kwenye mapinduzi haya, tukiwa wengine tunabaki nyuma ndiyo hao hao watakaotuvuta nyuma, inabidi wafuatiliwe, pengine tuwaulize kwa nini hawahuishi hizi taarifa,”aliagiza Jaji Mkuu.

Akiwa katika Mahakama hiyo, Mhe. Prof. Juma pia alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa kwake na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. John Chacha, ambaye ameeleza kuwa Mahakama yake na Mahakama za Mwanzo zinaendelea na zoezi la utoaji wa elimu kwa wananchi wanaofika mahakamani kuhudhuria mashauri yao kabla ya kuanza vikao vya Mahakama kila siku.

“Katika zoezi hilo wananchi wamepata fursa ya kufahamu taratibu mbalimbali za uendeshaji wa shughuli za kimahakama, kufahamu sheria na taratibu mbalimbali ambazo Mahakama inazitumia kuendesha mashauri,” Hakimu huyo alimweleza Jaji Mkuu.

Kabla ya kuongea na watumishi hao, Mhe. Prof. Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe. Abel Busalama, ambaye alimweleza changamoto mbalimbali zinazoikabili Mahakama ya Wilaya, ikiwemo uhaba wa watumishi, uchakavu wa majengo na ukosefu wa gereza, jambo ambalo huathiri kwa kiasi kikubwa kasi ya uondoshaji wa mashauri ya jinai.

Baadaye Mkuu wa Wilaya hiyo alimwongoza Jaji Mkuu kukagua ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya shillingi millioni 657 za Kitanzania ambalo kwa sasa lipo tayari kutumika na litakuwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja hadi Mei 2023.

Kabla ya kuhitimisha ziara yake leo, Mhe. Prof. Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe ambaye ameumwagia sifa uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kusimamia uboreshaji wa huduma za Mahakama, ikiwemo utoaji wa elimu ya kisheria kwa wananchi na kushughulikia mashauri kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo, Mhe. Mchembe alimwomba Jaji Mkuu kuingangalia Wilaya yake yenye Kata 33 kwa jicho la kipekee kwa vile ndiyo kubwa zaidi kuliko zingine mkoani Tanga na inachangamoto kubwa ya uhaba wa majengo ya Mahakama katika ngazi za Mahakama za Mwanzo na Mahakama ya Wilaya. Mhe. Prof. Juma alimwahidi kiongozi huyo wa Serikali kushughulikia changamoto alizoziainisha.

Baadaye, Mhe. Prof. Juma alipokea taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Wilaya ya Handeni kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Munga Sabuni, ambaye aliainisha mafanikio kadhaa yaliyofikiwa, ikiwemo kuongeza kasi ya uondoshaji wa mashauri hadi kufikia asilimia 35 kwa Mahakama ya Wilaya na asilimia 85 kwa Mahakama za Mwanzo.

Mafanikio mengine ni Mahakimu kuendelea kuchapa hukumu na mienendo ya mashauri wao wenyewe, usimamizi wa nidhamu kwa watumishi na kulipa stahiki zao kwa wakati, kuimarisha mahusiano na wadau wa Mahakama na kusajili mashauri kimtandao, kuhuisha taarifa katika JSDSII kwa wakati na kusajili na kuhuisha mashauri katika ‘Primary Court App’ kwa asilimia 87.

Katika siku ya tatu ya ziara yake, Jaji Mkuu anatarajia pia kutembelea maeneo mbalimbali ya Lushoto na Korogwe kabla ya kuhitimisha ziara yake Tanga mjini. Mhe. Prof. Juma ameongozana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba.

Wengine ni Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory Kagaruki, mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Bw. Yohana Mashausi, Afisa Utumishi, Bw. Jeofrey Mnemba, Mpima Ramani Abdallah Nalicho, Mhandisi Peter Mrosso na Msaidizi wa Sheria wa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Hassan Chuka.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa Mansoor, Naibu Msajili Beda Nyaki, Mtendaji Humphrey Paya, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Sofia Masati, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Mhe. Ruth Mkusi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Grace Mwaikono.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kilindi (hawapo kwenye picha) leo tarehe 17 Mei, 2022 katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor akitoa salamu mbele ya wafanyakazi wa Mahakama ya Wilaya Kilindi.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina akitoa utambulisho wa viongozi mbalimbali walioambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye ziara yake kwa watumishi hao.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokelewa kwa heshima na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe. Abel Busalama alipofika kumtembelea ofisini kwake.
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Mhe. Abel Busalama (kulia) akimwongoza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenda kukagua Mahakama ya Wilaya ya Kilindi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea taarifa ya ujenzi kutoka kwa Mhandisi Remen Shuma (kulia).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili katika Mahakama ya Wilaya ya Kilindi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kilindi, Mhe. John Chacha akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Mahakama hiyo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi Maria Itala akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na watumishi wakati wa kikao na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba (juu) na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory Kagaruki (chini) wakijibu baadhi ya hoja hizo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliosimama mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Handeni (picha juu na chini). Kulia kwa Jaji Mkuu ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor na kushoto kwa Jaji Mkuu ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina.

Post a Comment

0 Comments