Ticker

6/recent/ticker-posts

MHAGAMA AAGIZA IDARA YA RASILIMALIWATU KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO,MALIPO YA WASTAAFU



*************

Na Zena Mohamed,Dodoma.

WAZIRI wa nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora Jenista Mhagama,ameziagiza Idara za rasilimaliwatu kushughulikia malalamiko ya watumishi wastaafu kwa wakati yanayohusu ucheleweshwaji wa malipo yao.

Hatua hiyo ni kufatia kuwepo kwa malalamiko kuwa watumishi hao wanapostaafu wanapofuatilia haki zao ikiwa ni pamoja na nauli na gharama za kusafirisha mizigo baada ya kustaafu wanajibiwa kwa lugha mbaya za kukatisha tamaa na kueleza kuwa kitendo cha Mtumishi wa Umma kustaafu sio cha ghafla kiasi kwamba washindwe kufanya maandalizi ya kutosha na kusababisha malalamiko kwa Wastaafu.

Waziri huyo amesema hayo jijini hapa leo kwenye ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa idara za rasilimaliwatu katika utumishi wa Umma na kueleza kuwa hali hiyo inajidhihirisha kwa kuwepo na ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miiko ya kazi katika Utumishi wa Umma.

Amesema kumekuwepo na ucheleweshaji wa malipo nmna stahiki za wastaafu unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na kutowasilishwa kwa Michango na Tozo, Uwasilishaji wa nyaraka pungufu na wastaafu hivyo kuagiza idara hiyo kushughulikia sualq hilo kwa wakati na kuwaondolea usumbufu wastaafu hao.

Pia amesema ucheleweshaji huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na kutowasilishwa kwa Michango na Tozo, Uwasilishaji wa nyaraka pungufu na wastaafu kuwa na barua mbili tofauti za kupandishwa cheo na watumishi kupandishwa vyeo muda mfupi chini ya miazi sita (06) kabla ya kustaafu.

"Ninawaagiza kuhakikisha kuwa michango ya watumishi inawasilishwa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati na nyaraka zote zinazohitajika zinaandaliwa miezi sita (6) kabla ya mtumishi kustaafu na stahili za wastaafu zinazotakiwa kutolewa na Ofisi zenu zitengewe fedha katika bajeti za Ofisi zenu kila mwaka,"alisema

Hata hivyo amesema licha ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa, Utumishi wa Umma bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kushuka kwa uadilifu,nidhamu, kushuka kwa weledi, ubadhilifu na kutozingatiwa kwa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika kushughulikia masuala ya kiutumishi na Menejimenti ya Rasilimaliwatu.

Kutokana na hali hiyo Serikali imewahimiza Maafisa wa idara za rasilimaliwatu kuwajibika ipasavyo katika kushughulikia kwa wakati matatizo ya watumishi, kutoa ufafanuzi na ushauri wa masuala ya kiutumishi katika maeneo yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi zilizopo.

Amesema utumiaji mbaya wa madaraka, mali za umma ikiwemo magari ya Serikali, uzembe katika kutekeleza majukumu kunasababisha usumbufu kwa wananchi kwa kuwa kazi zinazofanywa na Watumishi wa Umma zinapaswa kuonekana na kuwagusa wananchi moja kwa moja.

"Kila mara ninapenda kuwakumbusha kuwa, rasilimali zote husimamiwa na Rasilimaliwatu hivyo ni muhimu kuhakikisha mnasimamia Rasilimaliwatu vizuri ili kuliwezesha Taifa kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi,zingatieni sana suala la nidhamu ya kazi na uwajibikaji,"amesema

Waziri Mhagama pia amesisitiza kuwa suala la uwazi na uwajibikaji ni msingi wa haki za binadamu na utawala wa Sheria na kwamba pamoja na hatua kubwa iliyofikiwa ya kujenga nidhamu katika utendajikazi na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma, bado wapo watumishi wachache miongoni mwao ambao hawawajibiki ipasavyo.

"Kwa mfano Ofisi yangu na mimi binafsi tunapokea malalamiko mengi kutoka kwa watumishi yanayo wasilishwa kwa barua, kwa kupiga simu, ujumbe mfupi wa simu (sms) na watumishi wengine kufika Ofisini ambapo baada ya kuwasikiliza na kupitia nyaraka wanazokuwa nazo inaonekana kuwa mengi kati ya malalamiko waliyonayo yangeweza kutatuliwa huko waliko, kimsingi matatizo mengi yanatokana na wahusika kutotimiza wajibu wao,"amesema.

Vilevile alisema, Ofisi yake imekuwa ikipokea maombi ya ufafanuzi wa maelekezo ya masuala mbalimbali ambayo yangeweza kutolewa na wasimamizi wa Rasilimaliwatu mahali walipo na kwamba ukiangalia kwa undani ni wazi suala la uwajibikaji limekuwa halitiliwi maanani katika sehemu za kazi.

Mbali na hayo amesema yeye kwa nafasi yake ataendelea kufanya uchambuzi wa malalamiko yanayowasilishwa na watumishi wa umma na Taasisi itakayobainika kuwa na watumishi wengi wenye malalamiko ambayo yanatakiwa kutolewa majibu na mwajiri; Mwajiri na Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Taasisi hiyo watakuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao, na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao kwa kuzingatia mamlaka yao ya nidhamu.




"Ninapenda kusisitiza kuwa, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Utumishi wa Umma sitamuonea huruma mtumishi mzembe, mwizi na mbadhirifu wa mali za umma,ninawataka mkasimamie Rasilimaliwatu kwa kuzingatia Kanuni za Maadili katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005,

Hakikisheni mnatoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanyakazi kwa uadilifu, kuwajibika mwa Umma, kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya Taarifa,nasi kwa kama Serikali kupitia Ofisi yangu tutaendelea kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha Viongozi na Watumishi wa Umma katika ngazi zote wanakuwa na malengo yanayopimika na yanayotekelezeka,"amesisitiza

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho Dkt. Laurean Ndumbaro amesema mkutano huo wa siku mbili utawaongezea maafisa hao ubunifu, weledi na uwajibikaji wa hiari katika usimamizi wa Rasilimaliwatu kwa ustawi wa Taifa .

"Katika siku hizi mbili tutapeana maelekezo mahususi kuhusu masuala mbalimbali ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia shabaha na vipaumbele vya Kitaifa,tunapofanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana katika nchi yetu, tunatambua mchango mkubwa wa watumishi wetu wa umma ambao wanafanya kazi kwa bidii, weledi na moyo wa uzalendo kwa nchi yao,"amesema.

Amesema mafanikio yanayoonekana katika nyanja za kiuchumi na kijamii yanaonesha weledi na ubunifu mkubwa unaofanywa na watumishi wa umma na kuongeza kuwa Serikali inajivunia huduma bora zinazotolewa na watumishi wa umma zikiwemo ujenzi wa miundombinu ambayo imesanifiwa na kusimamiwa na watumishi wa umma ikiwemo mifumo ya TEHAMA kama vile Mfumo mpya wa Taarifa za Watumishi wa Umma na Mishahara (NEW HCMIS) na miradi mikubwa ya Kitaifa.

Post a Comment

0 Comments