Ticker

6/recent/ticker-posts

OFISI YA MAKAMU WA RAIS KUTEKELEZA MRADI WA MAZINGIRA BUNDA


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Mei 18, 2022.

***************************

Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia utekelezaji wa Mradi wa Bunda Climate Resilience and Adaptation Project katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara ili kukabiliana na athari za ukame.

Hayo yamesemwa leo Mei 18, 2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma.

Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Bunda Mhe. Boniphace Getere aliyetaka kujua ni lini Mradi wa Mabadiliko ya tabianchi utawafikia wananchi wa Tarafa ya Chamriho wanaokabiliwa na tatizo la ukame.

Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Khamis alisema mradi huo utakaosimamiwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) una thamani ya Dola za Kimarekani 1,400,000 na unafadhiliwa na Adaptation Fund.

Alibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa wilayani humo katika maeneo ya Kata za Kasuguti, Namhura, Iramba, Neruma, Mahyolo, Igundu na Butimba kwa mujibu wa andiko lililoidhinishwa, hata hivyo Kata ya Chamriho kwa sasa iko nje ya mawanda (scope) ya mradi.

Aidha, naibu waziri huyo alisema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutafuta fursa mbalimbali za miradi ya Mazingira kwa kushirikiana na Halmashauri ya Bunda ili kukabiliana na changamoto iliyopo katika Tarafa ya Chamriho.

Kwa upande mwingine Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa alitaka kufahamu ni lini miradi ya mazingira itawafikiwa wananchi wa jimbo hilo kisiwani Pemba ambao wameathirika na changamoto za kimazingira.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuvuta subira wakati Serikali ikifanya mchakato wa kutekeleza miradi itayasaidia kuondosha changamoto hiyo.

Pamoja na hayo pia alitoa wito kwa wananchi kujiepeusha na shughuli za kibinadamu ambazo si rafiki kwa mazingira hasa ukataji miti ikiwemo mikoko hatua inayosababisha changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Alitoa wito kwa wabunge kuelimisha wananchi ili waone umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Post a Comment

0 Comments