Ticker

6/recent/ticker-posts

SMCCT LAWAKUTANISHA WADAU KUCHANGIA SH.MILIONI 5 KUSAIDIA WANAWAKE NA WASICHANA MKOANI SINGIDA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Save the Mother and Children of Central Tanzania (SMCCT), Evalyen Lyimo (katikati) akizungumza katika mkutano na wadau wakati wa utambulisho wa Mradi wa Wakuze Wanawake na Wasichana Kiuchumi (WAWAKI) katika hafla iliyofanyika hivi karibuni mkoani hapa.
Mjumbe wa Shirika hilo, Japhet Kalegeya akizungumza katika hafla hiyo.
Mjumbe wa Shirika hilo Michael Moses akichangia jambo kwenye hafla hiyo.
Mwakilishi wa Kanisa la Tanzania Assemblis of God akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwakilishi wa Mashirika Yasiyo ya kiserikali, Happy Francis akichangia jambo kwenye hafla hiyo.
Picha ya pamoja.


************************

Na Dotto Mwaibale, Singida


SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Save the Mother and Children of Central Tanzania (SMCCT) lenye makao makuu yake mkoani Singida limewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ili waweze kupata Sh. milioni 5 ili kuweza kusaidia Mradi wa Wakuze Wanawake na Wasichana Kiuchumi (WAWAKI)

Akizungumza hivi karibuni katika hafla fupi ya kuutambulisha mradi huo kwa wadau hao Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Evalyen Lyimo alisema mradi huo umelenga kuwakuza wanawake na wasichana kiuchumi ili kupunguza vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao na watoto.

Alisema mradi huo utawakuza wanawake kiuchumi kwa kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa kuwashirikisha wanawake na wasichana katika kilimo cha viazi lishe,alizeti na kilimo cha mbogamboga na kuwapa elimu ya usindikaji wa viazi lishe ili kuviongezea thamani pamoja na utafutaji wa masoko

" Mradi huu ukianza utawafikia wasichana 40 kutoka katika Kata tatu za Ihanja, Iseke na Ikungi Wilayani Ikungi Mkoa wa Singida ifikapo Mei, 2022" alisema Lyimo.

Lyimo alisema Wanawake na Wasichana toka Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida hawashiriki kikamilifu katika masuala ya kiuchumi kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto vinavyochangiwa na uelewa mdogo katika masuala ya usawa wa kijinsia, umasikini, kipato kidogo kwenye kaya na wanawake kutokuwa na uwezo wa kuchukua maamuzi katika kaya na jamii, usiri wa wanawake na wasichana kutomiliki mali zinazohamishika na zisizohamishika.

Alisema mradi huo utashughulikia changamoto ya kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kunakochangia wanawake na wasichana kutoshiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi.

"Takwimu za mwaka 2013 za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa asilimia 51 ya wanawake wa Mkoa wa Singida wamenyanyaswa kijinsia kutokana na mila kandamizi na potofu" alisema Lyimo.

Lyimo alisema ili kufanikisha mradi huo wanahitaji kupata Sh.milioni 5 ambapo aliwaomba wadau mbalimbali kutoka ndani ya mkoa wa Singida na mikoa mingine kusaidia kuunga juhudi hizo za kuwakwamua kiuchumi wanawake na wasicha kupitia mradi huo ambapo alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan, taasisi za dini, wafanyabiashara, mashirika ya umma na sekta binafsi, wanasiasa na wabunge na watu mbalimbali watakaokuwa tayari kutuma mchango huo katika Akaunti Namba 03120116510 Tawi la NBC.

Baadhi ya wadau walioalikwa kwenye hafla hiyo ni Benki ya NMB, CRDB, NBC,Wafanyabiashara, Shirika la SEMA, Mashirika Yasio ya Kiserikali na Madhehebu mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments