Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA MAMBO YA NJE AFAFANUA USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA CHOGM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alipongea nao kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022

Hotuba kamili ya Mhe. Waziri wa Mambo ya NjeTAARIFA YA MHESHIMIWA BALOZI LIBERATA MULAMULA (MB.), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA 26 WA WAKUU WA SERIKALI WA JUMUIYA YA MADOLA TAREHE 29 JUNI 2022.

Ndugu wanahabari, ninawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ... Kazi iendelee!!

Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo tukiwa na afya njema. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee kwa kufika kwenu. Ni matarajio yangu kuwa kupitia vyombo vya habari mnavyoviwakilisha, watanzania na dunia kwa ujumla itaweza kufahamu nilichopanga kukiwasilisha kwenu leo.

Ndugu Wanahabari, nimewaita hapa leo kuwapa taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 19 hadi 25 Juni 2022.

Kama mnavyofahamu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama hai wa Jumuiya ya Madola toka nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961 na imeendelea kuwa mwanachama baada ya Muungano mwaka 1964. Kufuatia uanachama huo, Tanzania imekuwa ikinufaika na kushiriki shughuli zote za Jumuiya hiyo.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliofanyika Kigali uliongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huu wa 26 umefanyika baada ya kuahirishwa mara mbili (2020 na 2021) kutokana na janga la UVIKO-19 ambalo linaendelea kuitesa dunia hadi sasa. Mojawapo ya mijadala ya mkutano huu ilikuwa ni namna gani dunia itakavyoweza kujikwamua kiuchumi na kijamii kutokana na janga hili.

Ndugu Wanahabari, Mkutano huu wa 26 ulihudhuriwa na Wakuu wa Serikali 27 kati ya nchi 54, ambapo wakuu wengine wa Serikali wapatao 27 waliwakilishwa. Mkutano ulifanyika chini ya kaulimbiu, “Delivering a Common Future: Connecting, Innovating and Transforming” ambayo ilijikita kwenye maeneo makuu ya kipaumbele ya utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu; vijana; afya; teknolojia na uvumbuzi; na uendelevu kwenye masuala ya uchumi, biashara, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira.

Ukichunguza vizuri maeneo hayo ya vipaumbele yanalingana kabisa na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita, kitu ambacho kilitusukuma kushiriki kwa nguvu kubwa katika mkutano huu.

Ndugu Wanahabari, Mkutano wa CHOGM ulikuwa na matukio mengi ambayo kutokana na muda, haitakuwa rahisi kuyaeleza hapa yote, hivyo, naomba mnipe ruhusa, ni yataje machache. CHOGM 2022 ilitanguliwa na mikutano kadhaa iliyohusisha Majukwaa ya Jumuiya ya Madola; mikutano ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, mikutano ya pembezoni (side events) na mikutano ya uwili (bilaterals meetings).Jukwaa la Biashara

Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la biashara ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili fursa za biashara na uwekezaji kwenye Jumuiya ya Madola na Bara la Afrika na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hizo zikiwemo athari zitokanazo na janga la Uviko-19 na mgogoro kati ya mataifa ya Ukraine na Urusi, uliongozwa na Dkt. Hashil Twalib Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Wajumbe wengine walitoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Benki za CRDB na KCB na Chama cha Wakulima wa Maua, Mbogamboga na Matunda (TAHA) na (CTI). Ujumbe wa Tanzania pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji kwenye Jukwaa hili, uliwasilisha kwa wawekezaji orodha ya miradi 115 iliyopo katika sekta mbalimbali nchini kwa ajili ya kutafuta wabia kwenye miradi hiyo kwa utaratibu wa Public Private Partnerships (PPP).

Jukwaa la Wanawake

Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la Wanawake (Commonwealth Women’s Forum) uliongozwa na Bibi Abeida Rashid Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Pamoja na ushiriki wa Serikali Asasi mbalimbali za Kiraia kutoka Tanzania nazo zilishiriki. Jukwaa hili lilijadili usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake kwenye nyanja zote; kuongeza nafasi za uongozi kwa wanawake; kutoa elimu bora kwa watoto wa kike na namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri haki za wanawake.

Jukwaa la Vijana

Vijana saba kutoka Tazania walishiriki Jukwaa la Vijana lililojadili masuala ya ajira kwa vijana, kuendeleza ujuzi na vipaji kwa vijana; elimu kwa vijana; kusaidia vijana wajasiriamali; matumizi ya teknolojia kwa vijana; kujiajiri; na kuongeza udhamini kwenye shughuli za vijana.

MIKUTANO YA MAWAZIRI

Ndugu Wanahabari, katika Mikutano hii, Mawaziri wa Mambo ya Nje, walikutana kwenye mikutano miwili: mmoja ulijadili Mkutano wa Wakuu wa Serikali na mwingine ulizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu nchi ndogo (small states).

Kwa upande wa Mkutano wa Mawaziri kuhusu nchi ndogo uliofanyika chini ya Uenyekiti wenza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na St. Vincent and Grenadines ulijadili changamoto za nchi ndogo hususan kufuatia janga la UVIKO-19, athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha za maendeleo.

Baada ya mkutano huo, iliazimiwa kutumia mkakati ujulikanao kama United Nations-Commonwealth Advocacy Strategy, kujenga ubia wa kukabiliana na changamoto zinazokabili nchi ndogo.

Mkutano mwingine wa Mawaziri wa Mambo ya Nje ulikikita kwenye kuandaa Mkutano wa Wakuu wa Serikali (Pre-CHOGM Commonwealth Foreign Ministers’ Meeting) kwa kujadili nyaraka mbalimbali za mkutano zilizopokelewa kutoka kwenye mikutano ya Maafisa Waandamizi na mkutano wa watendaji wakuu wa Serikali ambao ulihusisha Makatibu Wakuu-viongozi (Chief Secretaries).

Nyaraka hizo ni: matamko kuhusu usimamizi bora wa matumizi ya ardhi (Commonwealth Living Lands Charter РA Call to Action on Living Lands (CALL)), ukuaji endelevu wa miji (Declaration on Sustainable Urbanization) na huduma na ulinzi kwa watoto (Kigali Declaration on Childcare and Protection Reform). Vikao hivyo vilijadili pia Tamko la Mwisho la Mkutano(Communiqu̩).MKUTANO WA WAKUU WA SERIKALI WA JUMUIYA YA MADOLA

Ndugu Wanahabari, Ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola ulifanyika tarehe 24 Juni, 2022. Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mwana wa Mfalme wa Uingereza, Charles, The Prince of Wales, aliyemwakilisha Malkia Elizabeth II wa Uingereza ambaye ndiye Mkuu wa Jumuiya hiyo; Mhe. Rais Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha mwaka 2022-2024; Mhe. Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madola tangu mwaka 2018; Wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola walioshiriki CHOGM 2022; na baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama walioshiriki Mkutano huo.

Baada ya ufunguzi wa Mkutano huo, ulifanyika uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola. Wagombea waliojitokeza walikuwa ni Bi. Kamina Johnson Smith, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamaica na mgombea kutoka Tuvalu, Sir Iakoba Italeri, ambaye aliingia dakika za mwisho.

Baada ya raundi mbili za kura, Bi. Patricia Scotland alishinda kwa kupata kura 27 wakati Bi. Smith alipata kura 24 na Bw. Italeri alipata kura 3. Kwa matokeo hayo Bi. Scotland anaendelea kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki ya kukamilisha kipindi cha pili cha uongozi wake hadi mwaka 2024.

Ndugu Wanahabari, baada ya uchaguzi, Wakuu wa Serikali au wawakilishi wao walifanya vikao vya utendaji chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais Kagame. Niliiwakilisha Jamhuri ya Muungano ya Tanzania baada ya Mhe. Makamu wa Rais kurejea nyumbani kuendelea na majukumu mengine. Vikao hivyo vilijadili mada zifuatazo:

Mjadala kuhusu Mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria

Ndugu Wanahabari, chini ya mada hii, mkutano ulijadili umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuimarisha demokrasia, utawala bora, na kuheshimu mipaka kati ya mihimili mitatu ya dola ili kufikia mustakabali wenye usawa kwa wote. Ajenda hii ni muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Madola ikiwemo Tanzania kwa kuwa zinakabiliwa na changamoto katika maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazohitaji misingi mizuri ya demokrasia, amani na utawala bora kupata utatuzi wake.

Katika mjadala huu, Tanzania ilieleza umuhimu inaotoa kwa kanuni za utawala bora na utawala wa sheria tangu kupata uhuru. Vilevile, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kusaidia nchi wanachama kutekeleza programu za kukuza uelewa miongoni mwa watendaji wa taasisi za umma na binafsi ili kutambua majukumu waliyonayo katika kuhudumia wananchi, hivyo kuepuka rushwa na vitendo ambavyo vinakinzana na kanuni za utawala bora na utawala wa sheria.

Mjadala wa Maendeleo Jumuishi na Endelevu

Ndugu Wanahabari, mjadala chini ya eneo hili ulihusu kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanahusisha vipengele muhimu kuhusu utunzaji wa mazingira na ujumuishwaji wa makundi mbalimbali ya jamii nzima. Chimbuko la mada hii ni namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuathiri mafanikio ya nchi yaliyopatikana kupitia uwekezaji; pamoja na umuhimu wa makundi yote ya jamii kujumuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya nchi.

Tanzania ilisisitiza umuhimu wa vijana, wanawake na walemavu kujumuishwa kwenye sera za kitaifa na kimataifa kwenye kutunza mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza biashara na uwekezaji. Vile vile ilieleza ulazima wa nchi maskini zaidi duniani kushirikishwa kikamilifu na kwa usawa kwenye mfumo wa kibiashara wa kimataifa; na umuhimu wa nchi zinazoendelea kujengewa uwezo, kupatiwa teknolojia na fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.MIKUTANO YA PEMBEZONI

Ndugu Wanahabari, Wakati wa Mkutano wa CHOGM, kulifanyika mikutano mingine mingi ya pembezoni ambayo ilijadili nada mbalimbali. Mikutano miwli kati ya hiyo ilijadili Malaria na Magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Malengo ya Mkutano huu yalikuwa ni kupokea mikakati ya viongozi katika kukabiliana na malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Mhe. Makamu wa Rais alieleza changamoto kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kukabiliana na magonjwa haya wakati ambapo mapambano dhidi ya UVIKO-19 yanaendelea. Aidha, alieleza uzoefu, mafanikio na mikakati ya Tanzania kukabiliana na magonjwa hayo.Mkutano wa Kuzuia na Kupambana na Viashiria vya Ugaidi

Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu aliongoza ujumbe wa Tanzania ulioshiriki kwenye mkutano wa pembezoni kuhusu kuzuia na kupambana na viashiria vya ugaidi. Mkutano huu ulijadili athari kwa vijana na wanawake kutoka nchi za jumuiya, ambayo ni makundi yanayoathirika kwa kiasi kikubwa na madhara yanayotokana na masuala ya ugaidi. Mkutano huo ulianisha mikakati kadhaa ya kupambana na changamoto hiyo ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidigitali na kupambana na uenezaji wa propaganda za itikadi kali na ugaidi, hususani kwa vijana.

Tanzania ilishiriki mkutano huu kwa kuzingatia kuwa Sekretatarieti ya Jumuiya ya Madola imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi, Magereza na Kituo cha Kupambana na Ugaidi nchini kukuza uelewa na kujengea uwezo vyombo hivyo vya usalama kukabiliana na viashiria vya ugaidi nchini Tanzania na eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.

MIKUTANO YA UWILI

Ndugu Wanahabari, Mheshimiwa Makamu wa Rais na mimi mwenyewe tulifanya mikutano ya uwili na viongozi mbalimbali waliohudhuria mikutano hiyo. Lengo letu lilikuwa ni kuitangaza nchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za utoaji wa huduma kwa jamii.

Mhe. Makamu wa Rais alifanya mazungumzo na Bi. Melinda Gates, mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Melinda and Bill Gates. Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Makamu wa Rais aliishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kusaidia Tanzania katika kuboresha sekta ya afya ikiwemo kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kupitia tafiti na kujengewa uwezo.

Vilevile, Mhe. Makamu wa Rais alieleza ukubwa wa changamoto ya malaria nchini Tanzania ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 94 ya wananchi wapo kwenye hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo. Kadhalika, Mhe. Makamu wa Rais alifafanua jitihada za kukabiliana na malaria ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Mwaka 2021-2025 unaolenga kupunguza maambukizi ya malaria hadi kufikia chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025 na kutokomeza kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030. Aidha, alieleza upungufu wa bajeti uliopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 540 ili kutekeleza mpango huo kikamilifu.

Ndugu Wanahabari, mimi mwenyewe pia nilikuwa na mkakati maalum wa kutumia fursa ya mkasinyiko huo wa viongozi kufanya nao mazungumzo. Nilifanikiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina Rabbani Khar, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Amina Mohammed na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair.

Viongozi Wakuu niliokutana nao sio kwa mazungumzo rasmi, lakini nilifanikiwa kuwapa salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Mhe. Boris Johnson, Waziri, Mkuu wa Canada, Mhe. Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame; Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta; na Rais wa Nigeria, Mhe. Muhammadu Buhari.

Ujumbe wangu katika mazungumzo hayo ni kuhusu maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba Tanzania ni eneo salama kwa wawekezaji. Maeneo niliyosisitiza ni kilimo, utalii, afya na usafiri wa anga na Uchumi wa buluu hasa katika usimamizi na uendeshaji wa bandari na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Ndugu Wanahabari, baada ya kusema hayo, ninawashukuru sana kwa mwitikio wenu, na ni matarajio yangu kuwa mtatumia vyombo vyenu vya habari kueneza tarifa hii ili iwafikie wananchi.

Ndugu Wanahabari, nimalizie kwa kuwasalimu tena kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania……Kazi iendelee!!!
Post a Comment

0 Comments