Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. SHEMDOE AWAASA VIJANA KUWA WAADILIFU, WAZALENDO WANAPOTUMIKIA UMMA NA TAIFA

  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaasa vijana wa vyuo vikuu kuwa waadilifu na wazalendo pindi watakapoajiriwa Serikalini kuwatumikia wananchi au kupata fursa za uongozi wa kulitumikia taifa.

Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa vijana hao Juni 20, 2026, wakati akifungua Kongamano la Vijana (Youth Uongozi Forum) kwa niaba ya Mhe. Prof. Palamagamba John Aaidan Kabudi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu) ambalo linalofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro, lililoandaliwa na taasisi ya Tanzania Leadership Foundation (TLF).

“Vijana wangu, watoto wangu, wadogo zangu mjitahidi sana kuwa waadilifu na wazalendo kwani mkishindwa kuwa waadilifu na wazalendo hamtaweza kudumu katika nafasi mtakazoaminiwa kuzitumikia,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka vijana hao kuwa wanyenyekevu watakapopata fursa ya kuwahudumia wananchi kwani haitowagharimu chochote kumsikiliza na kumuhudumia vizuri mwananchi anayefuata huduma, na kuongeza kuwa hakutakuwa na tija yoyote kwa kijana kuwa na majivuno pindi akipata nafasi ya kuutumikia umma.

Aidha, Prof. Shemdoe amewahimiza vijana wote nchini kutokata tamaa, kutokatishwa tamaa, kuchukua hatua mapema (pro-active) kwa jambo lolote wanaloliona linaweza kuwasaidia badala kusubiri kuambiwa walifanye na kuongeza kuwa, vijana wanapaswa kuilinda nchi kwa hali na mali kwani hakuna taifa lingine ambalo watajivunia zaidi ya taifa mama ambalo ni Tanzania.

Prof. Shemdoe amewahikikishia vijana kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwajengea vijana mazingira bora kwa kuimarisha miundombinu ya elimu, mafunzo ya ujuzi pamoja na kuwawezesha kujikomboa kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini, hivyo amewataka vijana kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo huku wakiwa wanaendelea na masomo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewaasa vijana hao kutotegemea akili za watu wengine katika kujenga uwezo wao wa kufikiri bali watumie akili na uwezo wao binafsi katika kutafakari, kuchambua na kufanya maamuzi yenye mantiki, ili kujijenga na kuwa watu bora zaidi katika jamii.

Naye, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Taasisi ya Tanzania Leadership Foundation Mhe. Jabiri Makame ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe  amesema kuwa, msingi na dira ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutengeneza kizazi cha vijana viongozi ambao ni wazalendo, wenye maono, uwezo wa kujiongoza, kutoa uongozi katika taasisi za umma na sekta binafsi.










Post a Comment

0 Comments