Ticker

6/recent/ticker-posts

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA RAIS WA CARE INTERNATIONAL

Shirika lisilo la Kisekari la Care International limetakiwa kupanua huduma zake katika mikoa mingi zaidi badala ya mikoa tisa tu ambayo shirika hilo kwa sasa linatoa huduma zake hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Balozi Liberata Mulamula, wakati wa mazungumzo yake na Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Bi. Michelle Nunn

Bi. Nunn ametaja baadhi ya shughuli ambazo shirika lake inazifanya hapa nchini kuwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira, afya, elimu, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kilimo, haki za kijamii na usawa wa kijinisa. Amesema utekelezaji wa shughuli hizo umezingatia kipaumbele cha mwanamke.

“Tunasaidia watoto wa maeneo ya vijijini kupata elimu bora, tunasaidia jamii kutumia aridhi yao vizuri ili izalishe chakula, wakati huo huo ikitunzwa vizuri na programu zetu za kutoa mikopo na kuwasaidia wanawake wa vijijini kujiwekea akiba kwa kutumia teknolojia ya kiasasa ya kidigitali zimewawezesha wanawake wengi kumiliki rasilimali na kunyanyuka kiuchumi”, Alisema Bi. Nunn.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula alilishukuru shirika hilo kwa misaada inayotoa nchini na kueleza kuwa programu zao za misaada zinaenda sanjari na dira ya maendeleo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aliendelea kueleza kuwa changamoto kwa wanawake ni nyingi zikiwemo za afya ya uzazi na ugonjwa wa malaria ambao bado unakatisha maisha ya watu wengi katika nchi za Afrika, hivyo alishauri umuhimu wa “Care International” kuangalia kwa jicho la pekee eneo hilo.

Aidha, Balozi Mulamula alilipongeza shirika hilo kwa kujikita katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa na watu wengi hawalioni, ingawa madhara ya uharibifu wa mazingira yanamfikia kila mmoja wetu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo nchini Tanzania



Ujumbe ulioambatana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn ukifuatilia mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia) akiwa katika mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn huku maafisa walio chini yao wakifuatilia mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (katikati) akifurahia jambo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Care International, Bi. Prudence Masako
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Rais na Mtendaji Mkuu wa Care International, Bi. Michelle Nunn wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi walioambatana nao wakati walipofanya mazungumzo jijini Dar Es Salaam.

Post a Comment

0 Comments