Ticker

6/recent/ticker-posts

JAJI MKUU ASHAURI TAARIFA ZA ARDHI KUWEKWA BAYANA

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka bayana taarifa za ardhi na makazi kwa wananchi ili kuepuka ongezeko la migogoro ya ardhi nchini.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi leo tarehe 13 Julai, 2022 jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye ziara ya kikazi katika Divisheni hiyo, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, migogoro mingi ya ardhi inatokana na kutokuwa na taarifa sahihi za umiliki wa ardhi hali inayosababisha wananchi kuwa na migogoro ya ardhi ya mmiliki halali wa eneo husika.

“Pengine imefika wakati sasa taarifa zinazokusanywa na Wizara husika ziweze kupatikana kwa wananchi ili masuala ya ardhi yaweze kuwa wazi zaidi na yasiibue migogoro ambayo inachukua muda mrefu mahakamani,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amebainisha juu ya umuhimu wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kuangalia pia uwezekano wa kutumia Usuluhishi kama njia mojawapo ya kupunguza mlundikano wa mashauri ya Ardhi.

“Jambo lingine la kuangalia katika kupunguza migogoro ya ardhi ni suala la Usuluhishi, inabidi kuangalia uwezekano wa mashauri ya ardhi yaishie kwenye hatua ya usuluhishi ili yasichukue muda mrefu mahakamani,” ameongeza Mhe. Prof. Juma.

Ameongeza kuwa, ni muhimu Majaji kuisoma Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 2020 (Arbitration Act, 2020) ili kuangalia maeneo ambayo yanaweza kusaidia kupungua mashauri ya migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi, huku akiwasisitiza pia kutotumia kwa wingi vigezo vya kiufundi katika uendeshaji wa mashauri hayo ili kuondokana na kadhia ya mlundikano.

Jaji Mkuu ametoa mfano wa baadhi ya nchi ambazo zinatumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa mashauri mbalimbali kuwa ni pamoja na Singapore ambayo inatumia njia hiyo kwa asilimia 90 huku Marekani ikiwa na asilimia 60 katika matumizi ya usuluhishi. Ameongeza kuwa, njia hii husaidia pia kuleta amani na kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa amesema Divisheni hiyo imejipanga thabiti kuondoa mlundikano wa mashauri, akieleza kuwa, kuanzia mwezi Januari mwaka huu mpaka sasa jumla ya mashauri 914 yamefunguliwa katika Divisheni hiyo huku mpaka sasa Divisheni hiyo imesikiliza na kuamua jumla ya mashauri 1,271 (ikiwemo sehemu ya mashauri yaliyosalia kwa mwaka jana).

“Mahakama ya Ardhi imejipanga kwa dhati, kuondokana na mlundikano, na hii ni kutokana na uwajibikaji pamoja na ushirikiano wa dhati wa Majaji wa Divisheni hii, napenda kuahidi leo kuwa mpaka kufikia mwezi Novemba mwaka huu tutakuwa hatuna mlundikano,” amesema Jaji Agnes.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka 2021, Divisheni hiyo ilikuwa na mashauri yaliyobaki (pending cases) 2,246, mashauri yaliyofunguliwa (filed cases) 1,784 na mashauri yaliyoamuliwa (decided cases) yalikuwa 2,229.

Jaji Mfawidhi huyo, ameongeza kuwa katika kuunga mkono azma ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’, Divisheni inafanya kazi zake kwa nyingi kwa njia ya TEHAMA ikiwemo kusikiliza baadhi ya mashauri ya njia ya Mkutano Mtandao ‘Video Conference’.

Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma ameanza ziara leo maalum kwa ajili ya kutembelea Divisheni za Mahakama Kuu ambapo ameanza kwa kutembelea Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi na Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi. Katika ziara hii Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Watumishi wa maeneo hayo Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu isemayo Mapinduzi ya nne ya Viwanja; Safari ya maboresho kuelekea Mahakama Mtandao, hivyo amesisitiza kuhusu matumizi ya TEHAMA katika Mahakama ili kufikia azma ya kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’ ifikapo 2025.

Katika ziara yake ya siku nne (4) Mhe. Prof. Juma amepanga kutembelea Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na kuhitimisha ziara yake tarehe 20 Julai kwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi (hawapo katika picha) alipofanya ziara katika Divisheni hiyo leo tarehe 13 Julai, 2022.
Majaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Divisheni hiyo katika ziara yake ya kikazi. Wa kwanza kushoto ni Mhe. Isaya Arufani, wa pili kushoto ni Mhe. Victoria Makani, katikati ni Mhe. Dkt. Benhajj Masoud, wa pili kulia ni Mhe. Arafa Msafiri na wa kwanza kulia ni Mhe. Dkt. Theodora Mwenegoha.
Sehemu ya Watumishi wa Divisheni wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha)
Sehemu ya Watumishi wa Divisheni wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza nao.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza katika Mkutano kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi. Mhe. Siyani aliambatana na Jaji Mkuu katika ziaraaliyefanya ziara katika Divisheni hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Divisheni hiyo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania aliyefanya ziara katika Divisheni hiyo.
Meza kuu. Wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi.
Sehemu ya Watendaji na Wakurugenzi wa Mahakama walioambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipofanya ziara Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi. Wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Bi. Maria Itala, kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi-TEHAMA, Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili, Kurugenzi ya Malalamiko na Ukaguzi wa Huduma za Mahakama, Mhe. Aidan Mwilapwa na wa pili kushoto ni Bw. Matutay, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa (kushoto) akimpatia zawadi maalum Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya Jaji Mkuu kuhitimisha ziara yake katika Divisheni hiyo.
Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma akiifurahia zawadi yake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa (kushoto) akimpatia zawadi maalum Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani.


(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Post a Comment

0 Comments