Ticker

6/recent/ticker-posts

BENKI YA EXIM YAWEKA KAMBI LINDI,MTWARA,YATOA MSAADA WA MADAWATI,YAJIZATITI KUKUZA BIASHARA NA KILIMO


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti (kushoto walioketi) sambamba na viongozi waandamizi wa benki ya Exim akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Benki ya Exim, Stanley Kafu (katikati) Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (Kulia walioketi) na Mkuu wa Matawi ya Benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda(Kulia) wakiwa wameketi katika moja ya madawati 100 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania kwa ajili ya Mkoa wa Mtwara yakiwa ni sehemu kampeni ya ugawaji madawati 1000 yaliyofadhiliwa na benki hiyo kwa ajili ya shule za msingi katika mikoa mbalimbali nchini. Wengine ni maofisa wa mkoa huo, wafanyakazi wa benki hiyo na wanafunzi.


Mbunge wa jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, Mama Salma Kikwete (kushoto) akipokea msaada wa madawati 100 kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Benki ya Exim, Stanley Kafu (kulia) kwa ajili ya kusaidia kuondoa adha ya upungufu wa mawadati katika shule mbalimbali za jimboni kwake ikiwa ni sehemu ya mpango wa benki hiyo wa ugawaji wa madawati 1000 katika mikoa mbalimbalimbali hapa nchini kupitia mpango wake wa kusaidia jamii ujulikanao kama Exim Cares. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (wa tatu kulia)na maofisa wengine kutoka serikalini na benki hiyo.


Mbunge wa jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, Mama Salma Kikwete (kushoto) akitoa neno la shukrani kwa viongozi waandamizi wa benki ya Exim akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Benki ya Exim, Stanley Kafu (katikati walioketi), Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (wa pili kulia walioketi) wakati wakati wa makabidhiano ya madawati 100 yaliyotolewa na benki ya Exim Tanzania kwa ajili ya jimbo la Mchinga yakiwa ni sehemu kampeni ya ugawaji madawati 1000 yaliyofadhiliwa na benki hiyo kwa ajili ya shule za msingi katika mikoa mbalimbali nchini.


Wafanyakazi wa Benki ya Exim wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi watakaonufaika na msaada wa madawati 100 yaliyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya jimbo la Mchinga yakiwa ni sehemu kampeni ya ugawaji madawati 1000 yaliyofadhiliwa na benki hiyo kwa ajili ya shule za msingi katika mikoa mbalimbali nchini.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti akizungumza na wateja wa benki ya Exim mkoa wa mkoa huo wakati wa hafla ya chakula maalum kwa ajili ya wateja wa benki hiyo mkoani humo iliyolenga kutoa wasaa wa kujadili fursa za kibiashara, mipango ya ukuaji na huduma zitolewazo na benki hiyo katika mkoa huo.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti (wa pili kushoto) akibadilishana mawazo na baadhi ya wageni waalikuwa wakiwemo viongozi waandamizi wa mkoa huo pamoja na Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (katikati) wakati wa hafla hiyo.


Baadhi ya wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki ya Exim kutoka mkoa wa Mtwara wakiwa kwenye hafla hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti (katikati) akibadilishana mawazo na baadhi ya wageni waalikuwa wakiwemo viongozi waandamizi wa mkoa huo pamoja na Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (kulia) wakati wa hafla hiyo.


Wafanyakazi wa Benki ya Exim wakiwemo Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kutoka Benki ya Exim, Stanley Kafu (kushoto walioketi) Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo (wa pili kushoto walioketi) wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wateja wa benki hiyo mkoani Mtwara wakati wa hafla ya chakula maalum kwa ajili ya wateja wa benki hiyo mkoani humo iliyolenga kutoa wasaa wa kujadili fursa za kibiashara, mipango ya ukuaji na huduma zitolewazo na benki hiyo katika mkoa huo.

.................................

Lindi na Mtwara: Julai 25, 2022: Benki ya Exim Tanzania imeelezea adhma yake ya kukuza na kuchochea ukuaji wa kiuchumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kukuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kukuza sekta ya kilimo, biashara na elimu katika mikoa hiyo

Katika kuthibitisha adhma yake hiyo, viongozi waandamizi wa benki hiyo wakiwemo Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo pamoja na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Stanley Kafu mwishoni mwa wiki walitoa msaada wa madawati 200 katika mikoa hiyo sambamba na kuandaa hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya wateja wa benki hiyo Mkoani Mtwara.

Hatua hiyo ilitoa fursa kwa benki hiyo kuelezea huduma zake mpya, fursa za biashara pamoja na mkakati wake katika kukuza sekta za elimu pamoja na kilimo husasani kupitia zao la korosho.

Akizungumza kuhusu matukio hayo, Lyimo alisema yameweza kutoa fursa kwao kukutana na wateja wao, viongozi waandamizi wa serikali na wadau wengine muhimu mkoani humo hivyo kutoa wasaa kwao wa kutambulisha huduma mpya sambamba na kupokea mrejesho kuhusu mahitaji ya wateja wao hususani kipindi hiki ambacho mikoa hiyo ipo kwenye mkakati wa kuboresha zaidi sekta ya kilimo na bandari ya Mtwara.

“Mikoa ya Mtwara na Lindi ni miongoni mwa mikoa muhimu sana kwetu kibiashara na hiyo ndio sababu mikoa hii ilikuwa ni miongoni mwa mikoa ya awali kabisa kufungua matawi yetu. Katika kipindi chote cha uwepo wetu katika mikoa hii tumekuwa na mchango mkubwa kwa wakazi wa mikoa hii kwa kutoa huduma zinazowalenga haswa ikiwemo mikopo ya kilimo, biashara, mikopo ya watumishi na sasa tumekuja na huduma mahususi kwa ajili ya wajasirimali,’’ alisema.

Zaidi alisema hali ya uchumi katika mikoa hiyo kupitia uboreshwaji wa bandari ya Mtwara inazidi kutoa fursa kubwa kwa benki hiyo kuhudumia wateja wengi zaidi wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na wa kati kutoka ndani na nje ya nchi ambao wanatumia bandari hiyo.

“Uwepo wa benki ya Exim katika visiwa vya Comoro unatoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande hizi mbili kufanya biashara kwa urahisi zaidi kwa kuwa Exim tunawahakikishia huduma za uhakika za kifedha ikiwemo mikopo,’’ alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Stanley Kafu alisema mchango wa benki hiyo katika mikoa hiyo haujaishia katika utoaji wa huduma za kifedha tu bali pia imekuwa mdau muhimu wa maendeleo ya kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii ujulikanao kama Exim Cares

“Serikali kupitia viongozi mbalimbali wanafanya jitihada kubwa kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na kilimo hivyo ni jukumu letu sisi kama taasisi za kifedha kuunga mkono jitihada hizo za serikali. Kupitia mkakati huu uliozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwishoni mwa mwaka jana tumeweza kutoa msaada wa madawati katika mikoa mbalimbali hadi sasa ikiwemo mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Lindi na Mtwara na bado tunaendelea mikoa mingine zaidi.’’ alisema Bw Kafu.

Akizungumzia hatua hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliipongeza benki ya Exim kwa msaada wa madawati katika mkoa wake huku akibainisha kuwa msaada huo utasaidia katika kukabiliana na upungufu wa madawati katika baadhi ya shule zilizopo mkoani humo.

“Msaada huu umekuwa na tija kubwa kwenye mkoa wetu kwa kuwa tuna uhitaji wa madawati kutokana na muitikio mkubwa wa agizo la Mheshimiwa Rais la ujenzi wa madarasa. Tuna miradi mingi ya ujenzi wa madarasa ambayo inakwenda sambamba na hitaji la madawati hivyo tunawapongeza sana wenzetu wa Exim kwa kutuunga mkono kwenye hili,’’ alisema.

Kuhusu ukuaji wa biashara, Brigedia Jenerali Gaguti alisema uboreshwaji wa bandari ya Mtwara unaoshuhudiwa hivi sasa imekuwa ni kivutio kikubwa cha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo visiwa vya Comoros, hivyo wananchi wa mkoa huo wanahitaji huduma bora za kifedha ili waweze kushiriki kikamilifu kutumia fursa za kibiashara zitokanazo na uwepo wa bandari hiyo.

“Ndio maana nimeguswa sana kusikia kwamba benki ya Exim tayari imeshaanza kujitanua zaidi nje ya mipaka ya nchi. Tafsiri yake ni kwamba wafanyabiashara wetu na wale wanaotoka nje ya nchi ikiwemo visiwa vya Comoros tayari wanaunganishwa na huduma za benki ya Exim…hongereni sana.Ni matumaini yangu kwamba wafanyabiashara mkoani Mtwara watachangamkia zaidi huduma za Exim ili waweze kunufaika na huduma za benki hii wanapofanya biashara kimataifa,’’ alisema.

Akizungumzia msaada wa madawati 100 aliyoyapata kwenye jimbo lake, Mbunge wa jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, Mama Salma Kikwete pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake atahakikisha madawati hayo yanakabidhiwa katika Shule zenye uhaba na kutunzwa vyema kwa lengo la kuleta tija iliyokusudiwa hususani kukabiliana na uhaba uliopo unaotokana na mwitikio wa wazazi kupeleka watoto shule kufuatia sera ya elimu bila malipo.

Post a Comment

0 Comments