Ticker

6/recent/ticker-posts

BODI YA WADHAMINI - TANAPA YASISITIZA KASI UKAMILISHAJI MIRADI YA FEDHA ZA UVIKO-19


***********************

Na. Catherine Mbena/TANAPA

Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imesisitiza kasi ya ukamilishaji kwa wakati miradi iliyosalia katika Hifadhi za Taifa ili kutoa fursa ya kuongezewa miradi mingine kupitia Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara alisisitiza ukamilishwaji wa miradi michache iliyosalia alisema,

“Kwa ujumla tumeona kazi inavyoendelea vizuri, tumeridhika na tumeelekeza namna gani kazi hizi zikamilishwe kwa wakati. Mimi nihimize kwamba kazi hizi zikamilike kwa wakati uliopangwa bila kuwa na visingizio vyovyote. Wakandarasi wazingatie mikataba yao na kazi iwe yenye ubora uliokusudiwa”. Jenerali Waitara pia amepongeza ushirikiano na miongozo ya kitaalam ambayo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) wameutoa katika kuhakikisha kwamba viwanja hivi vinakuwa salama na kutoa huduma zinazokidhi viwango.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema alishukuru Bodi ya Wadhamini TANAPA kwa kutenga muda na kutembelea miradi ili kuona maendeleo na aliahidi kufanyia kazi maelekezo yote ya Bodi ili kukamilisha kazi kwa wakati.

“Sisi kama Menejimenti tumepokea maelekezo ya Bodi na kupitia wahandisi wetu tutawasimamia wakandarasi wote na kuhakikisha miradi katika hifadhi zote nufaika wa fedha hizi inakamilika kwa wakati kulingana na mikataba yao” alisema Mwakilema. Zaidi ya shillingi bilioni 46 zimetolewa kwa Hifadhi za Taifa kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Hifadhi ikiwa ni Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO–19 ambapo miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja na vivuko, ukarabati wa viwanja vya ndege, ujenzi wa barabara na njia za kupanda milimani na eneo la kutua helikopta za uokozi (Helipad), ujenzi wa malango ya ukusanyaji mapato, ununuzi wa mitambo na magari pamoja na ufungaji wa mifumo ya ufuatiliaji wa magari na mitambo.

Bodi ya Wadhamini TANAPA, imemaliza ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya uboreshaji miundombinu katika Hifadhi za Taifa Tarangire, Kilimanjaro na Mkomazi.

Post a Comment

0 Comments