Ticker

6/recent/ticker-posts

SHILINGI MILIONI 998/- KUPENDEZESHA MAENEO YA WAZI KATIKA HALMASHAURI YA TEMEKE


Matukio mbalimbali katika picha wakati Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akikagua maendeleo ya utekelezaji wa uboreshaji eneo la Mwembeyanga wilayani humo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mkakati wa kuboresha miundombinu na kupendezesha maeneo ya wazi na barabarani kwa kupanda miti na maua.

****************

Na Mwanadishi Wetu

WILAYA ya Temeke jijini Dar es Salaam imetenga zaidi ya Sh.milioni 998 kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha miundombinu katika maeneo ya wazi ikiwa pamoja na upandaji miti 1927 katika Wilaya hiyo.

Akizungumza alipotembelea eneo la wazi la Mwembeyanga ambapo vinajengwa Viwanja vya Michezo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo, amesema mradi huo ni sehemu ya lengo la Jiji la Dar es Salaam la kuboresha maeneo yake na kuyafanya kuwa ya kijani ' Green Dar'.

Jokate amesema mradi umeshaanza ambapo kwa sasa wanaboresha eneo la wazi la Mwembeyanga kwa kujenga viwanja vya michezo, upandaji miti maeneo hayo ya wazi, ukarabati wa mifereji kwenye baadhi ya barabara pamoja na kupanda miti na maua kwenye mfereji wa Serengeti na kandokando ya barabara ya Mtoni Kijichi kuelekea Toangoma ndani ya Manispaa hiyo.

" Kuhusu upandaji wa miti, miti 1427 itapandwa na Halmashauri katika maeneo hayo yaliyotajwa, miti 500 watapewa wananchi kwenda kupanda kwenye maeneo yao.Manispaa ya Temeke inatekeleza wa vitendo maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos ya Makala ya kutaka Jiji kuwa Safi na maeneo ya wazi ya kupumzika wananchi.

"Sasa pamoja na usafi tunaofanya, uwepo wa maeneo haya ya wazi yakiwa kwenye ubora mzuri si tu tutapendezesha Jiji, lakini pia tutakuwa tumewapa wananchi maeneo ya kupumzika.Mradi huo umewazingatia wakazi wa Halmashauri hiyo kwa kuwa baadhi ya vibarua ni wakazi wanaozunguka maeneo ya mradi huu,"amesema Jokate.

Aidha, amewataka wananchi wa Manispaa hiyo kutunza mazingira na miundo mbinu hiyo pindi mradi huo utakapokamilika.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo ambaye pia ni Meneja wa Wakala wa ujenzi wa barabara Mjini vijijini (TARURA) Manispaa Temeke, Injinia Paul Mhere amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo ulioanza wiki mbili zilizopita umefikia asilimia 25.

Amesema mara baada ya kukamilika ujenzi wa maeneo hayo ya wazi yatakuwa chini ya Halmashauri lakini wananchi hawatatozwa malipo kutumia maeneo hayo.

" Kwa wale waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika eneo la Mwembeyanga wataendelea na shughuli zao ingawa Halmashauri itaweka utaratibu mzuri na hakutakuwa na kiingilio."

Wakati huo huo Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya ukandarasi ya Group Six International Seleman Hamduni, amesema mradi huo utakamilika baada ya miezi miwili.

" Kazi kubwa kwenye maeneo haya ya Mwembeyanga ni ujenzi wa miundombinu ya maeneo haya ya wazi kama maeneo ya michezo, tumeanza na tumeshafikia asilimia 25 ya ujenzi wake, mkataba wa mradi huu ni miezi miwili na utakamilika kwa wakati," amesema.

Post a Comment

0 Comments