Ticker

6/recent/ticker-posts

Kutokomeza Malaria ni Kipaumbele cha Maendeleo kwa Afrika

Dar es Salaam, Mei 27, 2026 – Wakati Afrika ikiadhimisha Mwezi wa Afrika na kutafakari malengo ya Dira ya 2063 ya Umoja wa Afrika, wataalamu wa malaria wameitaka Afrika kuitazama vita dhidi ya malaria si tu kama changamoto ya afya ya umma, bali pia kama kipaumbele muhimu cha maendeleo kitakachoamua uimara na ukuaji wa baadaye wa bara hilo.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa, malaria inaendelea kuweka shinikizo kubwa kwa uchumi wa nchi za Afrika, mifumo ya elimu pamoja na miundombinu ya afya. Kwa mujibu wa ripoti ya malaria duniani ya mwaka 2025 ya World Health Organization (WHO), Afrika bado inabeba mzigo mkubwa wa malaria duniani, huku watoto walio chini ya miaka mitano na jamii zilizo katika mazingira hatarishi wakiwa waathirika wakubwa zaidi.

Mbali na athari za moja kwa moja za kiafya, maambukizi ya mara kwa mara ya malaria yanaendelea kuvuruga shughuli za kiuchumi, kupunguza uzalishaji na kuathiri maendeleo ya elimu katika nchi zilizoathirika. Watu wazima hukosa kazini mara kadhaa kwa mwaka kutokana na ugonjwa huo, huku watoto wakipoteza siku muhimu za masomo, jambo linaloathiri ujifunzaji wao na fursa za baadaye.

Mkurugenzi wa Programu ya Transmission Zero katika Ifakara Health Institute (IHI), Dr. Dickson Wilson Lwetoijera amesema kuendelea kwa malaria nchini Tanzania kunadhihirisha hitaji la mbinu mpya, uongozi wa Kiafrika na ushirikiano wa kimataifa wenye usawa.

Amesema kuna umuhimu wa kuwa na uwajibikaji wa pamoja, utaalamu wa pamoja na dhamira ya muda mrefu inayolenga kuhakikisha ubunifu unaendana na mazingira halisi ya ndani.

“Endapo tunataka ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, basi kutokomeza malaria lazima kubaki kuwa kipaumbele cha bara sambamba na kuendelea kuwekeza katika taasisi zinazoongoza tafiti za kisayansi barani Afrika,” amesema Dk. Lwetoijera.

Nchini Tanzania, taasisi kama Ifakara Health Institute (IHI) na National Institute for Medical Research (NIMR) zinaendelea kuongoza tafiti za kisayansi, maendeleo ya miundombinu ya ndani na uimarishaji wa ujuzi kwa lengo la kuimarisha jitihada za muda mrefu za kudhibiti malaria.

Ingawa mbinu kama matumizi ya vyandarua vyenye dawa, upuliziaji wa dawa ndani ya nyumba na matumizi ya dawa bora zimeokoa mamilioni ya maisha, changamoto zinazoongezeka za usugu wa dawa na viuatilifu zinaonyesha umuhimu wa kuendelea kubuni suluhisho mpya.

Kuongezeka kwa uwezo wa kisayansi katika nchi kama Tanzania kunaakisi mabadiliko mapana yanayoendelea Afrika, ambapo watafiti na taasisi za Kiafrika sasa wanazidi kushiriki katika kuongoza ubunifu wa afya kupitia uongozi wa kisayansi, ushirikiano wa kikanda na kimataifa pamoja na uwekezaji katika utaalamu na miundombinu.

Mkurugenzi Mwenza wa Transmission Zero na mtafiti mkuu wa kinga dhidi ya wadudu katika Imperial College London, George K. Christophides amesema mustakabali wa kutokomeza malaria Afrika haupaswi kuamuliwa kwa niaba ya Afrika.

“Afrika haipaswi kuwa eneo la majaribio na utekelezaji wa teknolojia mpya za afya ya umma pekee, bali pia iwe kitovu cha ubunifu, usimamizi na maendeleo ya teknolojia hizo kupitia taasisi imara za Kiafrika na ushirikiano wa kimataifa wenye usawa na uwajibikaji wa muda mrefu,” amesema.

Kwa upande wake, Dk. Lwetoijera amesisitiza kuwa suluhisho za baadaye za malaria lazima ziendelee kuongozwa na mifumo madhubuti ya utawala, usimamizi wa ndani wa kisheria pamoja na ushirikishwaji wa jamii.

Amesema Afrika ipo katika kipindi muhimu cha kihistoria, ambapo utekelezaji wa malengo ya Dira ya 2063 unaweza kufikiwa, lakini mafanikio hayo yatategemea maamuzi yanayofanyika sasa kuhusu maeneo ya uwekezaji, vipaumbele vya maendeleo na nani anayepaswa kuongoza safari hiyo.

Post a Comment

0 Comments