Ticker

6/recent/ticker-posts

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI ULANGA WAPIGWA MSASA KUHUSU BARUTI



***********

Ofisi ya Tume ya Madini Mahenge imeendesha mafunzo ya siku tano yaliyoanza mapema Julai 11, 2022 kwa wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli zao katika Wilaya ya Ulanga lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa namna bora ya matumizi ya baruti kwenye shughuli za madini.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mhandisi Migodi wa Ofisi ya Madini Mahenge, Eng. Joseph Ng'itu amewataka wachimbaji wadogo kuendelea kujifunza zaidi teknolojia ya ulipuaji na baruti ambayo imekuwa ikibadilika mara kwa mara.

Aidha, amewataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata cheti cha kulipulia na kusisitiza kuwa ofisi ya madini ipo tayari kutoa kwa watakaoomba.

Akizungumza kwenye ufungaji wa mafunzo hayo mapema leo Julai 15, 2022 Katibu Tawala wa Wilaya ya Ulanga, Abraham Mwaikwila amewataka washiriki wote kuzingatia yale waliyofundishwa hususan usalama wa matumizi ya baruti sambamba na kutekeleza Sheria na Kanuni za Baruti ipasavyo na kuachana na tabia ya kufanya shughuli za milipuko kimazoea pasipo kuzingatia utaalamu.

Katika hatua nyingine, amewataka wachimbaji wadogo hao kuwa mabalozi wazuri kwa wachimbaji wengine wadogo kwa kuwaelimisha Sheria na Kanuni zinazosimamia baruti ili nao waweze kutekeleza.

Katika hatua nyingine, ameipongeza Ofisi ya Madini Mahenge kwa kuandaa na kuratibu mafunzo hayo akiitaka Ofisi hiyo pia kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria wale wote wanaofanya shughuli za ulipuaji bila kufuata Sheria.

Post a Comment

0 Comments