Ticker

6/recent/ticker-posts

MGUMBA ATAKA MWEKA HAZINA KURUDI KUJIBU TUHUMA HALMASHAURI YA BUMBULI.

Watumishi na Madiwani wa halmashauri ya Bumbuli wakisikiliza na kuatilia kikao hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro akiongea na Watumishi pamoja na madiwani wa halmashauri ya Bumbuli.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akiongea na watumishi na Madiwani hao.


*********************************


Na Hamida Kamchalla, BUMBULI.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba ametoa agizo la kurudishwa aliyekuwa mweka hazina wa halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto Suleiman Said aliyehamishwa, kuja kujibu tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.

Mgumba ametoa agizo hilo baada ya kukutwa kwa mapungufu katika ofisi yake huku hakuna maelezo ya kujitosheleza kutokana na upotevu wa fedha hizo ambazo ziliingizwa na hazionekani kwenye mfumo.

Aidha Mgumba ametoa agizo hilo wakati alipokutana na viongozi pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo, na kumtaka mkuu wa polisi Wilaya ya Lushoto kufanya mawasiliano moja kwa moja katika Mkoa ambao amehamishiwa katika halmashauri yake.

"Nakuagiza Ocd, kesho ufanye mawasiliano na mkubwa wenu katika Mkoa aliohamishiwa hiyo mweka hazina ili asaidiwe kuletewa hapa aje ajibu hizi tuhuma na atueleze fedha hizo zimekwenda wapi kama hazionekani kwenye mfumo na matumizi yake hayajulikani" ameagiza .

"Kila mmoja atabeba mzigo wake, haiwezeiani watu wanafanya hujuma halafu tunachekeana, naomba fedha hizi zilizokuja kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ziende zikasimamiwe ziwanufaishe watu wa Bumbuni,

"Maelekezo yangu, miradi yote ambayo haijaanza katika halmashauri ya Bumbuli, ianze mara moja kuanzia kesho, na nina maanisha, nikija tena hapa nikakuta haijaanza anayewajibika hapa ndiyo nitaagana naye hapahapa" amesisitiza

Aidha Mgumba ameitaka halmashauri hiyo kuacha visingizio vya ukusanyaji mdogo wa mapato kutokana na kufa kwa kiwanda cha chai cha Mponde ambapo hapo awali mapato mengi yalikusanywa kupitia kiwanda.

Hata hivyo amebainisha kwamba ukusanyaji wa mapato unzorota kutokana na watendaji kutofanya kazi zao ipasavyo huku baadhi yao wakiishia kukusanya fedha hizo na kuweka mifukoni mwao.

"Kila mwaka halmashauri ya Bumbuli inakuwa ya mwisho katika ukusanyaji wa mapato, mlitoa kisingizio cha kufungwa kwa kiwanda cha Mponde, sasa kiwanda kinakwenda kufunguliwa mapema mwezi huu wa tisa, na tatizo hapa siyo kiwanda, tatizo ni uvivu wa wakusanyaji ambao wengine fedha zile wanaziweka mifukoni mwao" amebainisha.

Hata hivyo amemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuweka utaratibu mzuri wa kufunga hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali kwani tabia hiyo imejengeka na mara nyingi inasababisha ubadhirifu wa fedha na kutoa taarifa zisizokuwa sahihi katika matumizi ya fedha.

Amesema "mna tatizo la kutojibu hoja za mkaguzi wa ndani, tangu taarifa imeenda bungeni mwezi April, mpaka leo Bumbuli hoja nyingine hazijajibiwa na nyingine hazijafungwa, na mmekuwa na tabia ya kumuachia mkaguzi wa ndani na muhasibu kujibu hoja wakati walioanzisha hoja hizo ni idara zote"

"Mkurugenzi, hoja hazijibiwi na watu hawa pekee, bali zinajibiwa na watengeneza hoja wote, kama ni elimu ajibu mtu wa elimu, idara zote wakishajibu ndio muitishe kikao cha CMT na kupitia majibu yenu yote halafu ndiyo mtoe majibu kwa CAG, naomba hilo ulisimamie" amesema.

Naye mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro amesema kutokana na matumizi mabaya ya fedha za ufuatiliaji wa miradi, ameiagiza TAKUKURU kuchunguza ubadhirifu uliofanywa katika ufuatiliaji wa shule ya sekondari ya Hongoi ambapo kabla ya mradi kuanza fedha zimeshatumika na zimekwisha.

"Mimi nimeshamuagiza mtu wa TAKUKURU tangu juzi, kuna hela za kufuatilia, sh milioni 3 walitumiwa za ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa shule, jengo halijaanza tayari fedha yote imekwisha,

"Katibu Tawala Mkoa angalia, wamepewa fedha za ufuatiliaji wa miradi mingine sh milioni 18, vilevile kabla miradi Ile haijaanza fedha zile zimekwisha, kwahiyo kamati ya fedha mliochaguliwa juzi, kuweni wakali na matumizi ya fedha za miradi yasiyo sahihi" amesema.

Post a Comment

0 Comments