Ticker

6/recent/ticker-posts

MWENGE WAZINDUA MIRADI YA ZAIDI YA BILIONI 1 IKUNGI

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma (katikati) akivuta pazia kuashiria uzinduzi wa bomba la kusambaza maji ambalo limejengwa wilayani Ikungi mkoani Singida na Kampuni ya Chakwale kwa kushirikiana na RUWASA mkoani hapa kwa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali kupitia mapambano dhidi ya Uvico 19 katika hafla iliyofanyika jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa Ikungi, baada ya kuzinduliwa bomba hilo.
Mkimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru 2022, 'Birthday Boy' Sahili Nyanzabara Geraruma (kulia) akimlisha keki Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi
Kikundi cha Hamasa maarufu 'Nyakuanyakua' cha Wilaya ya Ikungi kikishiriki ipasavyo kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru eneo la Puma jana.
Taswira ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ikungi.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Ikungi wakisikiliza ujumbe maalumu wa Mwenge wa Uhuru 2022.

Na Godwin Myovela, Ikungi

MWENGE wa Uhuru umeridhishwa na utekelezaji ‘swadakta’ wa miradi mitano kwa sekta za elimu, maji, Barabara, utawala na maendeleo ya jamii-ambayo imegharimu takribani Shilingi Bilioni 1.4 zilizotolewa na serikali ndani ya Wilaya ya Ikungi mkoani hapa.

Miradi iliyopitiwa, kukaguliwa na hatimaye kuzinduliwa ni pamoja na mradi wa maji wa rafiki wa tenki kubwa na vituo vyake vya mtawanyo wa maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita zipatazo laki moja ambalo limejengwa na Kampuni ya Chakwale kwa kushirikiana na RUWASA mkoani hapa kwa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali kupitia mapambano dhidi ya Uvico 19.

Pia mwenge ulikagua na hatimaye kuridhishwa na ujenzi wa daraja la barabara ya Utaho-Makiungu lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja, mradi ambao unatekelezwa kwenye kijiji cha Minyinga kwa azma chanya ya kufungua fursa za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wakazi wa kata za Kituntu, Siuyu, Makiungu, Makotea na vijiji vingine jirani.

Aidha, fedha takribani shilingi 700 milioni zilizotumika kwa mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa halmashauri wilayani hapa ni kati ya miradi iliyoguswa na mwenge huo mwaka huu, utekelezaji ambao kukamilika kwake kunakwenda kupunguza umbali na uhaba wa malazi kwa watumishi na kuongeza ufanisi.

Zaidi, kiongozi wa ujumbe wa mbio za mwenge kwa mwaka huu, ‘Birthday Boy’ Nyanzabara Geraruma, kwa kushirikiana na wenzake Emmanuel Chacha, Rodrick Ndyamukama, Zadida Rashid, Grolia Peter na Ali Juma Ali walifurahishwa na kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ndani ya shule ya sekondari Issuna, mradi ambao umegharimu takribani shilingi milioni 41.

Pamoja na mambo mengine, mwenge wa uhuru kwa kauli mbiu ya ujumbe wa sensa kwa mwaka huu isemayo; “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa Tuyafikie Maendeleo ya Taifa” uliridhishwa na hatimaye kuzindua mradi mwingine wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Rushwa kwa mlengo wa ustawi wa elimu wenye shabaha ya kuleta matokeo chanya ya upatikanaji wa huduma zote bila rushwa.

Akizungumza jana baada ya kuzindua miradi hiyo, Geraruma aliwataka wakazi hao kuitunza miradi hiyo ambayo serikali imetekeleza kwa kutumia fedha nyingi, huku akisisitiza kasoro ndogondogo zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo zinapaswa kurekebishwa haraka kabla ya muda wa matazamio ya miradi husika.

Hata hivyo, kupitia ujumbe maalumu wa mwenge kwa mwaka huu, pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu mkubwa wa jamii kujitokeza kuhesabiwa kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi ifikapo Agosti 23 mwaka huu, ikizingatiwa msingi wa taarifa sahihi zitakazotolewa na wananchi baada ya matokeo rasmi ya sensa ndio utakuwa mwongozo kitakwimu utakaotumika katika mipango ya maendeleo kwa ustawi wa nchi.

Mwenge huo wa 2022, baada ya kupokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo Jerry Muro ukitokea Manispaa ya Singida hatimaye ulianza kukimbizwa katika umbali wa kilometa 112 kupita katika maeneo ya Tarafa za Mungaa, Ihanja na Ikungi, sambamba na kata 7 kati ya 28 na vijiji 17 kati 101 vilivyopo wilaya ya Ikungi kabla ya kukabidhiwa kuendelea na majukumu yake kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.


Post a Comment

0 Comments