Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI GEKUL AFUNGA UMITASHUMTA, AAGIZA SHULE BINAFSI KUSHIRIKI MICHEZO HIYO


*************************

Na Shamimu Nyaki. WUSM-Tabora

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameagiza Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia ushiriki wa Shule binafsi katika michezo ikiwemo mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA.

Mhe. Gekul ametoa rai hiyo leo Agosti 08, 2022 wakati akifunga Mashindano ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) mwaka huu katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, ambapo amesema michezo hiyo ni kwa ajili ya shule zote sio zinazomilikiwa na Serikali tu.

“Michezo ni muhimu, katika kuimarisha afya, kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, na inaleta upendo miongoni mwa jamii, nasisitiza mchakamchaka shuleni ufanyike, na somo la michezo pia lizingatiwe" amesema Mhe. Gekul.

Ameongeza kuwa, katika kuongeza wataalamu na waalimu wa michezo katika shule nchini, Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI katika ajira za walimu ilizotoa hivi karibuni, imeajiri pia waalimu 83 wa michezo na inatarajia kuongeza kadiri itakavyowezekana.

Mhe. Gekul amesisitiza waalimu kuwafundisha Wanafunzi nyimbo za uzalendo na Wimbo wa Taifa kwa usahihi bila kuingiza vionjo au kubadilisha nota za nyimbo hizo, huku akisisitiza matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili kwa wanafunzi.

Aidha, ameeleza kuwa, wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, zinaendelea kuboresha miondombinu ya Michezo kwa shule ambazo zimeteuliwa katika programu hiyo.

Hata hivyo, amewapongeza Wanafunzi wote ambao wameshinda makombe mbalimbali katika michezo hiyo, na kuwatia moyo wale ambao hawajashinda kujipanga kwa ajili ya mashindano yajayo.

Post a Comment

0 Comments