Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT.MPANGO AIAGIZA WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI KUKAMILISHA HARAKA BARABARA YA MCHEPUKO ENEO LA MLIMA WA INYALA MBEYA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitazama eneo lililotokea ajali na kusababisha vifo vya watu 19 na kujeruhi 25 mnamo Agosti 16, 2022 na ajali iliotokea tarehe 7 Septemba na kusababisha vifo vya watu 6 katika Kijiji cha Shamwengo kata ya Inyala mkoani Mbeya wakati alipotembelea eneo hilo leo leo tarehe 11 Septemba 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera (Kushoto) na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya Urich Matei (Kulia) namna ya kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na ajali za mara kwa mara katika mlima wa Inyala mkoani Mbeya wakati alipotembelea eneo hilo leo tarehe 11 Septemba 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kitengo cha Usalama Barabarani wa TANROADS Makao Makuu George Daffa (aliyevaa reflector) juu ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya ukaguzi wa magari katika eneo la Inyala mkoani Mbeya wakati walipotembelea eneo hilo leo tarehe 11 Septemba 2022.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiongozana na wananchi wa Kijiji cha Shamwengo kwenda kutembelea Zahanati ya Kijiji hicho inayojengwa na wananchi kata ya Inyala Mkoani Mbeya leo tarehe 11 Septemba 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitembelea na kujionea Zahanati inayojengwa na wananchi wa Kijiji cha Shamwengo kata ya Inyala mkoani Mbeya leo tarehe 11 Septemba 2022.

***********************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha inakamilisha haraka barabara ya mchepuko katika eneo la Mlima wa Inyala Kijiji cha Shamwengo mkoani Mbeya ili kupunguza matukio ya ajali yanayojitokeza mara kwa mara katika eneo hilo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipotembelea eneo la Inyala mahali zilipotokea ajali mbili hivi karibuni ka kusababisha vifo vya watu wapatao 25. 

Amesema Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.5 inapaswa kujengwa kiwango cha lami haraka kama suluhisho la muda mfupi litakarorahisisha upishanaji wa magari katika eneo hilo na kukabiliana na changamoto za ajali za mara kwa mara.


Halikadhali Makamu wa Rais amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Urich Matei kuhakikisha anasimamia ukaguzi wa magari yanayopita katika eneo la mlima wa Inyala ili kuepusha madhara ya ajali zinazojitokeza kutokana na ubovu wa magari hayo.


Aidha Makamu wa Rais ametoa siku kumi kwa Tanroads Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa miundombinu ya ukaguzi wa magari inayoendelea kujengwa katika eneo hilo ambalo linakabiliwa na changamoto za ajali mara kwa mara.

Makamu wa Rais amesema serikali inasikitishwa na madhara ya ajali yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka wahusika wakiwemo jeshi la polisi kutimiza wajibu wao kwa kuchukua hatua za kudhibiti ajali hizo zinazogharimu Maisha ya watu.

 Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo upanuzi wa barabara inayopita mkoani Mbeya kuanzia Igawa hadi Tunduma mkoani Songwe.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewasalimu wananchi wa Kijiji cha Shamwengo kilichopo kata ya Inyala ambapo amesema serikali itakamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji hicho ulioanza kujengwa na wananchi kwa kutoa shilingi milioni 100 za umaliziaji pamoja na kuchimba kisima katika eneo hilo ili kusaidia upatikanaji wa huduma za maji.

Makamu wa Rais amewapongeza wananchi hao kwa jitihada zao za kuanzisha mradi huo pamoja na moyo wao wa kujitolea katika kusaidia majeruhi wa ajali zinazotokea katika eneo hilo

Post a Comment

0 Comments