Ticker

6/recent/ticker-posts

KIKWETE AWATAKA VIONGOZI KUSIMAMIA MATUMIZI BORA YA ARDHI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete akiongea na viongozi na wakazi wa Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea kijijini hapo kukagua miradi ya ujenzi wa makazi yanayotumika kuhamishia kwa hiari wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha. Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga kukagua miradi ya ujenzi wa makazi yanayotumika kuhamishia kwa hiari wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati) akiwa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga kukagua miradi ya ujenzi wa makazi yanayotumika kuhamishia kwa hiari wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

***********************

Hassan Mabuye na Magreth Lyimo WANMM TANGA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Viongozi wa Wilaya ya Handeni na Mkoa wa Tanga kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo yao ili kuepuka migogoro ya ardhi isiyo ya lazima baina ya wananchi.

Kikwete alisema hayo tarehe 3 Septemba 2022 wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni Mkoa wa Tanga na kupokea taarifa ya miradi ya ujenzi wa kijiji hicho na kujionea kazi iliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita ya kuhamishia kwa hiari wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera.

‘’Zipo sheria ambazo zinasimamia mipango ya matumizi ya ardhi kwamba mji kabla haujaanza kujengwa na kuendelezwa unapangwa kwa kuwekewa matumizi ya ardhi mfano Msomera tumepanga maeneo ya michezo, shule, hospitali, malisho, majosho ya wanyama, masoko na maeneo mengine ya umma na binafsi hivyo nawataka viongozi wa mkoa na wilaya msimamie matumizi hayo kikamilifu’’ alisema Kikwete

Alisema kuwa katika kijiji cha Msomera Wizara ilipewa majukumu ya kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ambapo mipango hiyo ilitakiwa kuendana na shughuli zitakazo fanyika katika kijiji cha Msomera.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Omary Mgumba wakati akiwasilisha Taarifa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Ally Makoa alisema kwamba hadi tarehe 31/8/2022 wamepokea jumla ya kaya 183 za wakazi wangorongoro na kukabidhiwa nyumba 182 zenye jumla ya watu 1056.

‘’ Zoezi la kukabidhi nyumba linaenda sambamba na utoaji wa hati za hakimiliki za kimila katika viwanja na mashamba kwa kaya husika ambapo jumla ya hati za hakimiliki za kimila 355 zimetayarishwa ambapo hati kwa ajili ya makazi ni 176 na hati kwa ajili ya mashamba ni 179 ‘’ alifafanua Mgumba

Alisema kuwa zoezi la kuonyesha mipaka kwa kila kaya 183 zilizohamia kutoka Ngorongoro limekamilika kwa kuonyesha alama za mipaka ya viwanja na mashamba kwa wakazi waliohamia ambapo kila kaya imepatiwa eka 2.5 za makazi pamoja na eka 5 za mashamba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Makoa alikiri kuwa Msomera imepangwa vizuri na kamati imeridhika na kazi iliyotekelezwa kijijini hapo na kutoa wito kwa wananchi waliobaki ngorongoro wafike ili wajionee kazi iliyofanyika na Serikali.

Serikali inatekeleza mradi wa kuhamishia kwa hiari wananchi kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni. Wananchi hao walihamishiwa kijijini humo kwa kuwa eneo walilokuwa wakiishi awali limekuwa na changamoto nyingi za kiuhifadhi na maendeleo ya jamii zinazochangiwa na kuwepo kwa ongezeko la idadi kubwa ya watu, mifugo na shughuli za kibinadamu.

Post a Comment

0 Comments