Ticker

6/recent/ticker-posts

TARIS YAUNGANA NA JESHI LA POLISI KUZINDUA KAMPENI YA UTOAJI ELIMU YA USALAMA BARABARANI SHULENI

Mkurugenzi wa Taasisi ya Usalama Barabarani (TARIS), Bw.Maliki Barongo akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuelekea katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa elimu ya usalama barabarani. Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, Notker Kilewa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuelekea katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa elimu ya usalama barabarani.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

*********************

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

TANZANIA inaweza kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 endapo wadau na watumiaji wa barabara watatimiza wajibu wao wa kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani.

Ameyasema hayo leo Septemba 21,2022 Mkurugenzi wa Taasisi ya Usalama Barabarani (TARIS), Bw.Maliki Barongo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuelekea katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa elimu ya usalama barabarani.

Amesema yanayofanywa na taasisi hiyo ni kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi yote ikiwemo madereva wa magari na bodaboda, wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Amesema uzinduzi wa kampeni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Novemba 2021, huko mkoani Arusha akiwataka wadau kushirikiana na jeshi hilo kutoa elimu ya usalama barabarani hivyo waliona wawe wa kwanza kutekeleza agizo hilo.

Aidha, imesema Septemba 23, mwaka huu itafanya uzinduzi wa kampeni ya kutoa elimu katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari nchini, madereva wa magari, bajaji na bodaboda lengo likiwa ni kuyafikia makundi yote yanayotumia barabara.

''Baada ya ufunguzi huu tutapita katika shule mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu lengo kupunguza ajali za barabarani kwani hivi karibuni kumekuwa na ajali nyingi zinazohusisha wanafunzi na makundi mengine,''

Aidha amesema ajali za barabarani zimekuwa zikisababisha kupotea kwa nguvu kazi, gharama kubwa za kurekebisha miundombinu na majeruhi wanaopelekwa hospitalini.

Ameeleza kuwa TARIS inawajibu wa kushirikiana na serikali ili kufikisha elimu hiyo kwani asilimia kubwa ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu hivyo wanapaswa kuwakumbusha watumiaji wa barabara wajibu wao katika kupunguza ajali.

Pamoja na hayo amesema madereva kupitia mafunzo kwenye vyuo pekee hayatoshi badala yake wanapaswa kupata elimu ya mara kwa mara ili kufuata sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, Notker Kilewa amesema Jeshi la Polisi lina jukumu kubwa la kulinda usalama wa raia na mali zao hata wakati zinapotokea ajali.

‘’Tunajukumu la kutoa elimu kwa makundi yote yanayotumia barabara kama vile madereva, watembea kwa miguu, abiria, wasukuma mikokoteni na wanafunzi ili kubadili tabia zao na kutii sheria zilizowekwa. Ajali zimeendelea kujitokea kwa sababu ya mapungufu,’’ alisema Kilewa.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Tosh, Bw.Mohamed Nassoro amesema wataendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanafuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali.

Amesema ajali zinaacha wajane, yatima na kuleta hasara kwa taifa na jamii kwa ujumla hivyo watahakikisha elimu wanayoitoa inawafikia watu wengi jambo litakalosaidia nchi kuwa salama.

Post a Comment

0 Comments