Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZAZI NA WALEZI NCHINI WATAKIWA KUHAKIKISHA WANAWAANDIKISHA WATOTO SHULE WENYE UMRI WA KUANZA AWALI


*********************

Ofisi ya Rais TAMISEMI imewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha kuwa wanawaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza Elimu ya Awali (miaka 3-5) na wenye miaka sita kwa Elimu ya Msingi.

Hayo yamesemwa leo tarehe 12/09/2022 na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu, OR- TAMISEMI, Bwana Efrahim Simbeye katika ukumbi wa St.Gasper jijini Dodoma, alipokuwa akifungua m Mpango wa wiki 12 wa Mafunzo ya wawezeshaji wa Walimu Wasaidizi Jamii wa kuandaa mtoto kuwa ja Utayari wa kuanza shule. Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na TAMISEMI kupitia Programu ya Shule Bora.

Amesema kuwa ni lazima kwa watoto wote waliotimiza umri huo kuandikishwa ili kupata haki yao ya elimu.

“Natoa agizo la watoto wote wenye umri wa kuandikishwa shule kuanzia ngazi ya awali hadi msingi kuandikishwa kwani wapo watoto ambao hawajapata nafasi ya kuanza masomo hayo hivyo wazazi na walezi wahakikishe wanawaandikisha” amesema Bwana.Simbeye.

Amesema kuwa uandikishaji wa watoto umeanza mwezi huu Septemba na unatarajiwa kumalizika mwezi Desemba na mwakani mwezi Januari watoto wote wanapaswa kuanza shule na kwamba wanatarajia kuvuka lengo la uandikishaji la asilimia 103 iliyofikiwa mwaka 2021.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TET, Bwana. Moses Ziota amesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia watoto ambao walipaswa kuwa katika madarasa ya awali lakini walishindwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile umbali wa kutoka nyumbani ama kuishi katika mazingira hatarishi

Mafunzo haya yanashirikisha Walimu 57 kutoka katika mikoa mitatu ya Pwani, Simiyu na Rukwa ambapo baada ya mafunzo haya watakwenda kuwawezesha Wasaidizi Jamii wa Walimu ambao watawasaidia watoto kujenga umahiri na utayari wa kuanza shule.

Post a Comment

0 Comments