Ticker

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA-RAIS DKT. SAMIA ANATAKA KUONA SEKTA YA MIFUGO IKILETA MAPINDUZI YA KIUCHUMI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Siku Mbili wa Wadau wa Sekta ya Mifugo kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma, Disemba 19, 2022. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angela Kairuki na wa tatu kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Siku Mbili wa Wadau wa Sekta ya Mifugo kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma, Disemba 19, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*********************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana mapenzi ya dhati na Sekta ya Mifugo na anatamani kuona inaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kukuza zaidi pato la wananchi, kutoa ajira na kuchangia pato la Taifa bila kuathiri mazingira na maendeleo ya sekta nyingine.

Kutokana na dhamira hiyo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya maeneo ya ufugaji yaliyopo katika maeneo yao na kiasi cha mifugo kinachoweza kufugwa na endapo mifugo itazidi uwezo wa eneo husika, wafugaji waelekezwe kuvuna mifugo yao.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa maelekezo hayo leo (Jumatatu, Desemba 19, 2022) alipofungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa Sekta ya Mifugo unaofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma wenye dhima isemayo “Mwelekeo Mpya wa Sekta ya Mifugo Nchini.

“Wafugaji wahamasishwe kuvuna mifugo yao kwa wakati ili kuwawezesha kupata bei nzuri sokoni pamoja na kupunguza changamoto za malisho hususan wakati wa ukame. Kwa ujumla kasi ya uvunaji wa mifugo nchini bado ipo chini ya asilimia 10 ikilinganishwa na viwango bora vya uvunaji wa mifugo kitaifa ambavyo ni kati ya asilimia 20 na 25.”

Waziri Mkuu amezielekeza Wizara ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta ya mifugo katika kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji na kutenga maeneo ya malisho ya pamoja, ranchi za vijiji na vitalu kwa ajili ya wafugaji binafsi.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa vijiji vyenye ardhi ya kutosha, vitenge maeneo ya Ranchi za Vijiji zenye ukubwa wa kati ya hekta 200 na 500 ambazo zitatumika kwa utaratibu wa kuwapanga wafugaji kutoka ndani ya kijiji husika.

“Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo inamiliki Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ihakikishe maeneo yote ya NARCO yaliyoko kwenye mikoa yetu, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kwanza mtambue maeneo hayo yanamilikiwa na nani na mjue yapo katika wilaya gani na yana ukubwa upi na je matumizi ni sahihi kama Serikali inaotaka.

Kwa sababu tuna watu binafsi wamechukua ardhi hiyo kazi yao ni kukodisha watu wengine, tumewaacha wafugaji wenye ng'ombe na tunawajua huyu ana ng'ombe wake 200 huyu ana ng'ombe wake 300 na tuna eneo la NARCO zuri tu badala ya kumpa hyu mwenye ng'ombe tumempa mtu ambaye hana ng'ombe tumempa mtu ambaye hana ng'ombe alafu anakuja kumpangisha mwenye ngombe. Hii Wakuu wa Mikoa tuikatae wazi.”

Pia, ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau na wafugaji kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa ufugaji ikiwemo ufugaji wa kukaa katika eneo moja bila kuhamahama na wafugaji kulima malisho badala ya kutegemea malisho ya asili peke yake.

“Viongozi na watendaji wa Serikali, hakikisheni mnashirikiana kwa karibu na wadau wakiwemo wafugaji katika kuwekeza na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho, malambo, visima vya maji na maeneo ya malisho.”

Waziri Mkuu amesema kuwa uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo sambamba na kuwahamasisha wafugaji kutumia mifugo bora iliyofanyiwa utafiti na kuonesha kuwa na tija zaidi.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameelekeza wizara husika kuimarisha huduma za ugani kwenye sekta ya mifugo kwa kuweka vigezo vya kupima utendaji kazi na kuwafuatilia Wagani wote nchini ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya TEHAMA, kuendelea kuwapatia vyombo vya usafiri na mafunzo rejea kuhusu teknolojia mpya za ufugaji wenye tija na wa kibiashara.

Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishirikiane na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Pia wafugaji waelimishwe na kuhamasishwa kufuga kulingana na maeneo waliyonayo na kufuata sheria za nchi.

Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema lengo la mkutano huo ni pamoja na kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya mifugo kujadili kwa kina na uwazi kuhusu mwelekeo mpya wa sekta ya mifugo nchini na kuwajengea uwezo wafugaji ili wafuge kwa tija na kibiashara kama wawekezaji kwenye sekta ya mifugo.
Pia, Waziri Ndaki alisema Sekta ya Mifugo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo watatumia mkutano huo kujadili namna ya ufugaji bora pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. “Tumepanga namna ya kuwafikia wafugaji na kuwaelimisha juu ya matokeo ya athari hizo kwani sehemu kubwa ya mifugo imeathirika.”

Post a Comment

0 Comments