Ticker

6/recent/ticker-posts

MATUKIO YA MAUAJI WILAYA YA MANYONI WANANCHI WAMLILIA RC SERUKAMBA AWASAIDIE

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyoni na Itigi katika kikao cha kusikiliza kero kilichofanyika juzi wilayani humo.


Na Dotto Mwaibale, Singida

UTARATIBU wa ziara aliounzisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba kwenda kusikiliza kero za wananchi katika wilaya zote mkoani hapa zimekuwa na tija kubwa kwani zimeibua mambo mengi yakiwemo matukio ya mfululizo ya kuuawa kwa watu wilayani Manyoni.

Mauaji ya mfululizo ya watu ambao maiti zao zinaokotwa kila wiki maeneo tofauti ya Wilaya ya Manyoni yamewashtua wananchi wa wilaya hiyo ambao wamelazimika kupaza sauti kumweleza Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba, kumuomba aingilie kati na kuwasaidia kuliondoa jambo hilo.

Katika hali ya kushangaza,wananchi hao wamesema mauji ya watu ambayo yameibua hofu kubwa kwa jamii baadhi ya pikipiki zinazomilikiwa na askari polisi wa Manyoni kwa ajili kuendesha biashara zao ndizo zinatumika kwenye mauaji hayo.

Wananchi wa Manyoni walimweleza juzi hayo Mkuu wa Mkoa wa Singida,Serukamba ambaye alikwenda katika wilaya hiyo kusikiliza kero mbalimbali ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake zakusikiliza kero.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hapa Manyoni vifo vimekithiri sana kila wiki lazima tuokote maiti mahala fulani lakini sio kwamba wananchi wa Manyoni hawawafahamu wahalifu bali wanawafahamu ," alisema Prisca Maleta.

Maleta ambaye wakati akizungumzia suala hilo mamia ya wananchi waliokuwa kwenye kikao hicho walikuwa wakimshangilia, alisema wananchi wanashindwa kutoa taarifa polisi kutaja wanaohusika na uhalifu huo kwasababu baadhi ya polisi sio waaminifu wanaficha siri za watoa taarifa.

"Tatizo linakuja kwa Jeshi la Polisi mimi kama Prisca ninapokwenda kutoa taarifa polisi kabla mtuhumiwa hajaenda kukamatwa wanampa taarifa kuwa fulani amekuja kukuripoti huku,vitengo hivi ndio vinasababisha vifo kuongezeka kwasababu kunakuwa na visa na visa," alisema.

Maleta alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kuna baadhi ya askari ambao anawajua kwa sura na majina ambao wanamiliki pikipiki zao ambazo ndizo zinazoshiriki kwenye uhalifu wa mauji ya watu.

"Kuna baadhi ya askari kwa sura na majina ila siwezi kuwataja hapa ila ukihitaji nitakutajia wana pikipiki zao ambazo ndizo zinashiriki kwenye uhalifu," alisema.

Mwananchi mwingine Khalfan Zuberi Paloto alilalamikia jeshi hilo kitengo cha upelelezi kuwa mtu anapopeleka mashitaka kituoni na kufunguliwa jadala, badala ya kukutanishwa na askari mpelelezi wa kesi yake hupewa namba ya simu na kila ikipigwa muhusika husema yupo nje ya wilaya.

“Mimi nilipeleka kesi ya wizi nikapewa namba ya simu ya mpelelezi nilipompigia akataka nimpe namba ya simu ya mshukiwa, alipigiwa simu akimuita kituoni lakini mshukiwa alipofika hakumkuta ayelimuita,” alisema.

Paloto alisema tatizo hilo limekuwa sugu kwenye idara ya upelelezi ya polisi wilayani humo, hali inayowafanya waamini huduma haziwezi kuwa na ubora unaotakiwa kutokana na unyeti wa idara hiyo.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Manyoni (OCD), Ahmad Makele akijibu madai hayo alikiri kuwepo kwa mauaji hayo ya mara kwa mara wilayani humo.

"Vifo vinavyotokea sio vya kisasi wala kuwania mali sababu mtu akiuawa vinachukuliwa viungo vya mwili wake kama vile sehemu za siri," alisema.

Makele alisema Jeshi la Polisi limeanza kuchukua hatua za kukabiliana na mauaji hayo na watu kadhaa wamekwisha kamatwa na misako zaidi bado inaendelea kufanyika ili kukomesha vitendo hivyo.

Kufuatia malalamiko hayo ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Serukamba amemwagiza Afisa wa Usalama wa Taifa wa Wilaya ya Manyoni (DSO), kuunda kamati itakayoshirikisha vyombo vyote vya usalama kuchunguza mauaji hayo.

Serukamba ambaye alionekana kuchukizwa na suala hilo alisema mkoa anaoungoza hawezi kukubali kuwa na askari wanaoshirikiana na wahalifu.

"Haiwezekani watu wanauawa kirahisi rahisi na serikali ipo, vinginevyo tumwambie IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini) awaondoe Manyoni,pia hatuwezi kuwazuia na polisi wanaoshirikiana na wahalifu, hatuwezi kuwafukuza kazi lakini tunaomba wapelekwe mikoa mingine hapa tunahitaji kuona polisi wema ambao wanalinda wananchi na mali zao," alisema.

Alisema Jeshi la Polisi linao uwezo wa kuwajua wahalifu,washirikina na wanaofukua makaburi hivyo wote wafahamike wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa akizungumza katika kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mlagaza, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mkazi wa Manyoni Prisca Maleta.akitoa kero yake mbele ya mkuu wa mkoa.
Mkazi wa Manyoni Khalfani Zuberi akinyoosha kidole kuomba apewe nafasi ya kutoa kero zake.
Mkazi wa Manyoni Khalfan Zuberi akitoa kero zake.
Meneja wa Tanesco Wilaya ya Manyoni Mhandisi James Mushi akizungumza katikakikao hicho wakati akitoaufafanuzi kufuatia kero zilizokuwa zikiwasilishwa na wananchi.
Kero zikitolewa mbele ya mkuu wa mkoa.
Kikao cha kero kikiendelea.

Post a Comment

0 Comments