Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI KIKWETE AKEMEA UDANGANYIFU KATIKA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete (kushoto) akitoa maelekezo kuhusu mgogoro wa ardhi wa kijiji cha Ngage wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara mbele ya mbunge wa jimbo la Simanjiro Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Makongoro Nyerere.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Makongoro Nyerere akimuongoza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa kutembea ndani shamba lenye mgogoro katika kijiji cha Ngage wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara. Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ngage wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete kuhusu mgogoro wa ardhi unaomkabili mbunge wa jimbo la Simanjiro Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka na Nancy Yese ambaye ni mtoto wa rafiki wa mbunge huyo.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ngage wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete kuhusu mgogoro wa ardhi unaomkabili mbunge wa jimbo la Simanjiro Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka na Nancy Yese ambaye ni mtoto wa rafiki wa mbunge huyo.

********************************

Na. Hassan Mabuye, Manyara

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amekemea udanganyifu katika kutatua migogoro ya ardhi na kutaka wananchi walio na migogoro kukaa chini na kutumia busara kabla ya kufika hatua za kisheria na Kiserikali.

Kikwete ameyasema hayo jana katika kijiji cha Ngage wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakati alipofika kusikiliza na kutatua mgogoro wa ardhi unaomkabili mbunge wa jimbo la Simanjiro Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka na Nancy Yese ambaye ni mtoto wa rafiki wa mbunge huyo na kugundua kuna udanganyifu ndani yake.

“Nilichogundua hapa kuna udanganyifu maana mmesema Yese hakuwa na nyumba wakati tumeenda na tumeikuta, sasa nikuombeni sana kutaneni wenyewe malizaneni, kaeni kwenye meza zungumzeni na kama kuna jambo mnalihitaji katika ardhi hii mtaliweka wazi na kulitatua hasa ikizingatiwa nyinyi ni ndugu na marafki wa karibu maana sisi tukija ni kuamua kwa mujibu wa sharia” Alisema Kikwete.

Naibu Waziri kikwete alifika katika eneo hilo ili kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la ekari 3,500 ambalo linadaiwa kumilikiwa na familia ya marehemu Mzee Yese ikiongozwa na binti yake Nancy Yese huku baadhi ya wakazi wakiongozwa Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka wakidai Yese anamiliki sehemu tu ya shamba hilo isiyozidi ekari 500.

Awali baadhi ya wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Mheshimiwa Ole Sendeka walikanusha madai ya watoto wa mzee Yese kwamba baba yao alijenga nyumba na kuishi katika eneo hilo ili kuthibitisha umiliki wa shamba hilo.

Kutokana na madai hayo Mheshimiwa Kikwete aliamua kuzuru kwa kutembea kwa miguu kwa zaidi ya saa 3 ndani ya shamba hilo ili kujionea kwa macho yake baadhi ya vithibitisho vya umiliki wa shamba hilo na kukagua makazi na nyumba iliyodaiwa ni ya Yese.

Katika hali ya kustaajabu yalikutwa mabaki ya nyumba ambayo imechorwa na kusainiwa na mzee Yese ambaye ni mmiliki wake tarehe 21/11/2001 jambo lililompelekea Mheshimiwa Kikwete kuamini kuna kuna udanganyifu katika mgogoro huo wa ardhi kwani baadhi ya wakazi hao walidai eneo hilo halina nyumba kitu ambacho hakikua na ukweli ndani yake.

Katika kumaliza mgogoro huo wa ardhi Naibu Waziri Kikwete aliwataka wakazi hao wakiongozwa na Mbunge wao kukaa pamoja na familia ya Yese kwa uwazi na ukweli na kama wanahitaji eneo hilo kwa ajili ya ufugaji, malisho au kilimo basi wakubaliane na familia hiyo badala ya kulumbana.

Post a Comment

0 Comments