Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI INAVYOWAFUNGULIA FURSA ZA AJIRA VIJANA


Na Mwandishi Wetu, DODOMA

VIJANA 97,000 nchini wamenufaika mafunzo ya uanagenzi yanayotolewa kupitia programu ya kukuza ujuzi iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu inayolenga kufungua fursa nyingi za ajira kwa vijana.

Akizungumza jana jijini hapa namna serikali inavyozalisha fursa za ajira, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi wa Ofisi hiyo, Ally Msaki, alisema mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2017 kwenye vyuo vya ufundi 92 nchini na yanagharamiwa kwa asilimia 100 na serikali.

Alisema mwaka 2017 Tanzania iliandaa mwongozo wa mafunzo ya uanagenzi ili vijana wapate ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.

“Mwaka 2022 Tanzania ilishiriki mkutano mkuu wa Shirika la Kazi duniani(ILO) na kuandaa mwongozo wa mafunzo ya uanagenzi kimataifa hii ilitokana na kuwa nchi ya mfano kwenye uanagenzi na Tanzania ilitakiwa kutoa uzoefu wake wa mafunzo haya ambayo asilimia 60 ya muda wa mafunzo mtu anatakiwa kufanya akiwa eneo la kazi,”alisema.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo ni ya miezi sita na fani zinazotolewa ni ufundi umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, useremala, ufundi magari, umeme wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, upishi, uhudumu wa hoteli na vinywaji, ushonaji, uchenjuaji wa madini, ufundi bomba, ufundi uashi, uwekaji wa terazo na marumaru, ufundi viyoyozi na majokofu.


Alifafanua kuwa kwa mwaka 2022/23 vijana 11,975 wanatarajia kupata mafunzona hadi kufikia Januari, 2023 vijana 7,760 wamepatiwa ujuzi huku wengine 4,215 wakitarajiwa kuanza mafunzo mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu.


Kadhalika, Msaki alisema katika kuhakikisha vijana hao wanaunganishwa na mitaji kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana ili kujiajiri kwenye fani walizopata ujuzi.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2022/23 tayari fedha Sh.Bilioni 1.5 zimeshakopwa na vijana waliomaliza mafunzo,”alisema.


Hata hivyo, alisema ili kuwapatia vijana ujuzi wa kitaalaamu zaidi wameamua kufungua vituo atamizi katika mikoa minne ya Dar es salaam, Lindi, Singida na Kigoma.

“Vijana wanaopata mafunzo ya kutengeneza bidhaa ile tunawapa muda wa kuja kutumia vifaa vilivyokuwepo kwenye jengo la serikali tunachokiita kituo atamizi, atafanyia shughuli zake pale anakuja na mtaji wake, malighafi zake na pale kutakuwa na mtaalamu wa kumsimamia anakuja anafanya shughuli aliyojifunza mwenyewe, anazalisha inakuwa na viwango vinavyohitajika,”alisema.

Post a Comment

0 Comments