Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA NA LATVIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amewakaribisha wawekezaji kutoka Jamhuri ya Latvia kuja nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Kilimo na TEHAMA.

Balozi Dkt. Shelukindo ametoa wito huo leo tarehe 10 Machi, 2023 alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kumsalimia na kumpongeza kwa kuteuliwa hivi karibuni kwenye wadhifa huo.


Amesema Tanzania inayo ardhi ya kutosha kwa uwekezaji wa kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara hivyo wawekezaji kutoka Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri kwenye sekta ya kilimo duniani wanakaribishwa.


“Nimefurahishwa na ziara yako hapa Tanzania. Latvia ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika sekta ya kilimo duniani. Tunaunga mkono ushirikiano na Tanzania kwenye sekta hiyo na tunawakaribisha wawekezaji wenye tija kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususan kilimo na TEHAMA ” alisema Balozi Dkt. Shelukindo.


Awali akizungumza kwenye Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa baina ya Tanzania na Latvia, Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Latvia na kwamba majadiliano hayo ambayo yanalenga kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili, yamekuja wakati muafaka kwa nchi hizi mbili ili kuziwezesha kujiwekea malengo na mikakati mipya ya kuuimarisha ushirikiano ambao ulikuwa hafifu miaka ya nyuma.


“Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Latvia na tunapongeza uamuzi wenu wa kuja ili kama nchi mbili rafiki tuzungumze na kukubaliana namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu”, alisema Balozi Mndeme.


Aidha, amesema Tanzania kupitia ushirikiano na nchi za Umoja wa Ulaya ikiwemo Latvia imeendelea kunufaika kupitia sekta za biashara, utalii na uwekezaji huku akitoa mfano wa sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa imewavutia watalii wengi kutoka nchi za Ulaya kwa takribani asilimia 80 ya watalii wote wanaoingia Tanzania.


Amesema katika medani za kimataifa hususan agenda ya Mabadiliko ya Tabianchi, Tanzania inazisisitiza nchi zilizoendelea ikiwemo Latvia kutimiza ahadi yao ya kuchangia kiasi cha Dola za Marekani Bilioni Moja kila mwaka ili kuziwezesha nchi zinazoendelea ikwemo Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto na ukame.


Naye, Bw. Jansons ameeleza utayari wa Serikali ya Latvia wa kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali za manufaa kwa pande mbili na kusisitiza kuwa nchi hiyo ina mpango wa kuteua Mwakilishi wa Heshima wa nchi hiyo hapa nchini ili kushughulikia masuala yote ya ushirikiano.

“Naunga mkono hoja zote tulizojadiliana ikiwemo ya kuzikumbusha nchi zilizoendelea kutimiza ahadi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Latvia inayo nia ya dhati ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwa manufaa ya pande hizi mbili,” alisema Bw. Jansons.


Kupitia majadiliano hayo, Tanzania na Latvia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za Kilimo, Tehama, Utalii, Biashara na Uwekezaji, Mazingira na Uchukuzi hususan kwa kuimarisha matumizi bora ya Bandari.


Pia nchi hizi mbili zimedhamiria kusaini Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya Anga (BASA) baada ya majadiliano ya awali kukamilika kwa ajili ya kukuza Utalii na Biashara baina ya pande mbili; Kuunganisha Vyuo Vikuu vya Kilimo vya pande mbili kwa ajili ya kukuza matumizi ya teknolojia katika sekta ya Kilimo; na Kuunganisha Taasisi Kuu za Biashara na Uwekezaji za pande mbili kwa lengo la kukuza Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Latvia ambapo hivi karibuni ujumbe wa Wawekezaji kutoka Latvia watafanya ziara ya kikazi nchini kwa ajili ya kufahamu na `kutumia fursa za Biashara zilizopo nchini.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akizungumza na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons alipomtembelea ofisi kwake jijini Dodoma tarehe 10 Machi 2023. Pamoja na mambo mengine Viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Latvia

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Dkt. Shelukindo na Bw. Jansons hawapo pichani

Mazungumzo yakiendelea


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo akimpatia Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Latvia, Bw. Nils Jansons zawadi ya mchoro wa picha ya wanyama watano mashuhuri "Big Five" inayotangaza utalii wa Tanzania.




Post a Comment

0 Comments