Ticker

6/recent/ticker-posts

AJIRA MPYA 231 ZA RAIS SAMIA KUTATUA KERO ZA TEMBO- MCHENGERWA

Na John Mapepele


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaelekeza watendaji wa Wizara yake kuhakikisha kuwa askari wote wapya wapatao 231 wa uhifadhi waliohitimu leo Aprili 26,2023 mafunzo ya awali ya kijeshi katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi ya Jeshi la Uhifadhi (JU) Mlele, Mpanda mkoani Katavi, waende mara moja kwenye maeneo korofi ili kudhibiti wimbi la Wanyama waharibifu kwa kuhakikisha wanadhibitiwa na kurudishwa hifadhini.

Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira hizo mpya na kutoa miongozo mbalimbali inayosaidia uhifadhi wa raslimali na kuwa mstari wa mbele kutangaza utalii kiasi cha yeye mwenyewe kucheza filamu ya Royal Tour ambayo imeleta mageuzi makubwa nchini kwenye sekta ya utalii.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hizo leo wakati akifunga mafunzo ya awali kwa askari wenye ajira mpya 231 wa jeshi la uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi ya Jeshi la Uhifadhi (JU) Mlele, Mpanda mkoani Katavi ambapo ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi ambaye aliwatunukia vyeo askari wawili wa jeshi la uhifadhi, Abel Masota na Carloline Malundo kuwa Naibu Kamishna.


Pia wakati akimkaribisha Mhe. Mchengerwa atoe hotuba yake, Dkt Abbasi alitoa taarifa kuwa wahitimu hao wote watapatiwa barua zao leo leo za kuripoti katika vituo vyao vya uhifadhi na kwamba hiyo ni dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kazi iendelee.


Mhe. Mchengerwa amewataka askari hao wakawe wabunifu na kutanguliza uzalendo huku akiwaasa kutumia mbinu za kijeshi walizofundishwa ili kulinda kikamilifu raslimali zilizopo na kuepusha madhara makubwa inapotokea uvamizi wa aina yoyote kwenye maeneo ya Hifadhi.





" Na kwa kuwa jukumu hili la udhibiti ni la kila mmoja wetu (Serikali na Wananchi) ninawaagiza wakuu wote wa hifadhi nchi nzima kujipanga kikamilifu kwa kuweka mikakati thabiti na endelevu la kukabiliana na Wanyama hao wakali na waharibifu, shirikianeni na wananchi kutoa elimu na nyenzo kwa VGS za kukabiliana nao” amesisitiza Mhe. Mchengerwa


Pia amewaasa wahifadhi kushuka chini kwenye jamii na kutoa elimu kuhusiana na uhifadhi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na dini mbalimbali pamoja na viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii ili akiwepo mwanananchi anayekaidi achukuliwe sheria.

Amewatia moyo wananchi wote ambao wanaishi maeneo jirani na hifadhi kuwa Serikali yao ipo pamoja nao katika kuhakikisha kuwa changamoto zote za uvamizi wa Wanyama wakali na waharibifu zinatatuliwa katika kipindi kifupi kijacho.

“ Pia leo tunapoadhimisha miaka 59 ya Muungano wetu ni kipindi tunachoona Serikali yetu tukufu ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha uhifadhi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwahimiza wananchi kuhama maeneo haya kwa hiyari na kuwatafutia makazi mbadala na bora. Jambo hilo limeleta tija sana katika uhifadhi wa eneo hilo” amefafanua Mhe. Mchengerwa


Aidha, ameonya tabia ya baadhi ya wahalifu ya kujivika cheo cha “wananchi” na kufanya uhalifu ambapo amesema sheria itachukua mkondo wake ambapo pia amewaonya wananchi ambao wanavamia maeneo ya hifadhi na kuwataka kuondoka mara moja kwa kuwa maeneo hayo yaliyohifadhiwa ni kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.


Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) Prof. Dosantos Silayo akizungumza kwa niaba ya Watendaji Wakuu wa Taasisi bza Uhifadhi zilizo chini nya Wizara hiyo amemweleza Mhe. Mchengerwa kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na uhifadhi.

Ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoj a na kuimarika kwa uhifadhi, kuongezeka kwa maeneo ya uhifadhi, kuongezeka kwa upandaji wa miti na mashamba ya misitu pamoja na kuwepo kwa miundombinu ya utalii ambayo imesaidia kuwavuta watalii kutembelea katika maeneo hayo.

Chuo cha Mafunzo ya kijeshi Mlele ni chou kilicho chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kinatoa mafunzo ya kijeshi kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi.




Post a Comment

0 Comments