Ticker

6/recent/ticker-posts

DC SERERA AKABIDHI POLISI JAMII CUP 2023 KWA POLISI MIRERANINa Mwandishi wetu, Mirerani


Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Hassan Serera amewakabidhi mabingwa wa Polisi Jamii CUP 2023 Simanjiro, kombe na shilingi milioni moja, timu ya soka ya Polisi SC ya Mirerani baada ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.


Timu ya Polisi SC iliutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya mpira wa miguu kwenye viwanja vya Tanzanite Complex stadium, (Kwa Mnyalu) kwa kuifunga timu ya Tanesco FC mabao 4-3 ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 kwenye dakika 90.


Hata hivyo, timu ya soka ya Nyumba ya Mungu FC ilishika nafasi ya tatu baada ya kuifunga mabao 4-2 ya penalty timu ya Terrat SC kwenye mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu, baada ya dakika 90 kutoshana nguvu kwa bao 1-1.


Mkuu huyo wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Serera, akizungumza kwenye fainali ya michuano hiyo amewapongeza polisi kwa kuanzisha michezo hiyo ambayo kwa namna moja au nyingine imechochea burudani.


“Pamoja na Polisi SC kutwaa ubingwa nawapongeza timu ya Tanesco FC kwa mchezo mzuri ila baada ya kupata bao moja mkabweteka na kuruhusu bao likasawazishwa mkashindwa kwenye penalti siku nyingine mjitahidi mfunge mabao mengi zaidi ili mshinde mapema,” amesema Dkt Serera.


Amesema kupitia mashindano hayo, kutasababisha kupunguza uhalifu, kupiga vita dawa za kulevya na mmomonyoko wa maadili, kutokana na ujumbe uliokuwa unatolewa kwenye michuano hiyo.


“Mfano hapa mji mdogo wa Mirerani, kuna wanawake wanafanya biashara ya dawa za kulevya, hivyo wanatakiwa kuachana nayo na kufanya biashara nyingine,” amesema Dkt Serera.


Mkuu wa polisi wa wilaya ya Simanjiro, Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP), Mathayo Mmari akizungumza kwenye michuano hiyo, amesema mashindano hayo yenye lengo la kupinga vitendo vya ukatili na matukio mengine ya uhalifu eneo hilo.


SSP Mmari amesema kwa kupitia falsafa ya Polisi Jamii na ulinzi shiriki itasaidia kuiweka jamii karibu na polisi, jambo litakalowezesha kupata taarifa za uhalifu kwa urahisi na kuwaondoa wananchi hofu iliyojengeka kwa polisi.


Amesema timu 18 zimeshiriki mashindano hayo kupitia vituo vinne vya Orkesumet, Mirerani, Ngorika na Terrat, ambapo kituo cha Okresumet kulikuwa na timu za Young Stars, Red Fire, Tanesco FC, Veteran, Eagle FC, Young Boys, Bodaboda na Mkumbi SC.


“Timu zilizoshiriki kituo cha Mirerani ni mabingwa wa mashindano haya Polisi SC, Tanzanite Sports Academy, Vipaji FC na New Vision,” amesema SSP Mmari.


Ametaja timu zilizoshiriki kituo cha Ngorika ni Nyumba ya Mungu FC, Majengo SC, Chemchem FC na Kiruani FC ya Msitu wa Tembo na kituo cha Terrat ni Sukuro FC, Terrat SC na Komolo Rangers.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemey Laizer, amewapongeza washiriki wote wa michuano hiyo na kuwakabidhi washindi wa watatu timu ya soka ya Ngorika motisha ya shilingi 300,000.


Mkuu wa kituo cha polisi Okresumet, Mrakibu wa polisi (SP) Christina Mkonongo amesema kupitia mashindano hayo wametoa elimu juu ya polisi jamii, ulinzi shirikishi, kupiga vita mmommonyoko wa maadili na kutawaepusha vijana kuacha tabia za matumizi ya dawa za kulevya, bangi na ulevi ambavyo huchangia kuzorotesha uchumi wa nchi.


SP Mkonongo amesema wameandaa mashindano hayo ikiwa ni utaratibu uliopo chini ya IGP Camillius Wambura lengo likiwa kutoa elimu juu ya tabia hatarishi na vijana kuwa na afya bora kupitia michezo.


Diwani wa Kata ya Ngorika, Albert Msole ameipongeza timu ya Nyumba ya Mungu FC kwa kushika nafasi ya tatu kwenye michuano hiyo na kumshukuru Mwenyekiti wa CCM Simanjiro, Kiria Laizer kwa kuwapa wachezaji wake motisha ya shilingi 300,000 ya kununua soda.


Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer ameupongeza uongozi wa polisi kwa kuanzisha michuano hiyo ambayo imechangia vijana wengi wa wilaya ya Simanjiro kushiriki mchezo wa mpira wa miguu.

Post a Comment

0 Comments