Ticker

6/recent/ticker-posts

NACTVET YATOA MAFUNZO ELEKEZI KWA WAJUMBE WAPYA WA BODI ZA MASOMO


Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt. Adolf Rutayuga leo tarehe 12 Aprili, 2023 amefungua rasmi mafunzo elekezi kwa wajumbe wapya wa Bodi za Masomo katika ofisi za Baraza Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Rutayuga amewapongeza wajumbe hao wapya kwa kuaminiwa na kuteuliwa kushika nafasi hizo ili kusaidia kuendesha shughuli za Baraza. Bodi hizo za Masomo zinazoundwa na Baraza la Uongozi la NACTVET ni pamoja na Bodi ya Sayansi na Teknolojia Shirikishi, Bodi ya Afya na Sayansi Shirikishi na Bodi ya Biashara, Utalii na Mipango.

Lengo kuu la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajumbe juu ya sheria, kanuni, taratibu, na miongozo inayotumika kusimamia na kuratibu elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi; na kuwapa uelewa juu ya muundo mpya wa Baraza ili kurahisisha utendaji kazi wao. Pamoja na majukumu muhimu yaliyo mbele yao, wajumbe hao wamehimizwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na Baraza wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Aidha, wajumbe hao wapya wamepata nafasi ya kupitishwa kwa njia ya mawasilisho kile kinachosimamiwa na kila Kurugenzi na Vitengo vya NACTVET, ili wafahamu kazi na majukumu ya kila Kurugenzi na Vitengo hivyo, na wamepata nafasi ya kujadili na kupata ufafanuzi kutoka kwa Wakuu wa Kurugenzi na Vitengo husika.

Kwa upande wao, Wenyeviti wa Bodi za Masomo, wameushukuru Uongozi wa Baraza kwa kutoa mafunzo hayo na wameahidi kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.

Post a Comment

0 Comments