Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS DKT. MWINYI AIASA JAMII KUENDELEA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA KUKUZA JAMII YENYE MAADILI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia baada ya kumalizika kwa Fainali za Mashindano ya kusoma Qur-an Tartiil Zanzibar, zilizofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 19-4-2023.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akifuatilia Mashindano ya Fainali ya kusoma Qur-an Tartiil Zanzibar, yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 19-4-2023, na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Saleh Omar Kabi na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman.(Picha na Ikulu)


******************

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi aliiasa jamii kuendelea kuwajengea uwezo vijana ili kukuza jamii yenye maadili mema na hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu (S.W.)

Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye halfa ya mashindano ya Quran tukufu kwa njia ya Tartil yaliyofanyika ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa ndege Zanzibar.

Alisema kumekuwa na mporomoko wa maadili na kupotea kwa sehemu kubwa ya mila na silka za Wazanzibari, hivyo alieleza kupitia utaratibu wa kuwahifadhisha vijana Quran tukufu ni njia ya kuzalisha viongozi bora wa baadae wakiwemo Masheikh na Maulamaa.

Alisema hatua hiyo pia inahamasisha jamii juu ya kuendelea kukisoma kitabu kitukufu cha Qur’an ambacho ndani yake kuna faida nyingi zikiwemo kukisoma, kukisomesha na kukihifadhi.

Katika halfa hiyo, pia Al hajj Dk. Mwinyi alitoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa kila mshindi, kwa washindi watano wa mwisho ikiwa ni zawadi za ushiriki wao kwenye mashindano hayo, pia aliitaka jamii iendeleze kuhamasisha vijana wengi kwenye mashindano yajayo ili kukisoma vyema kitabu kitakatifu cha Qur’an.

Vile vile, Al hajj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuziomba sekta binafsi kuungana na sekta za umma kutoa mapema mshahara wa mwezi Aprili mwaka huu baina ya leo (Aprili 19) na kesho (Aprili 20) ili kuwapa muda wa kutosha wafanyakazi wao kwa maandalizi ya sikukuu ya Eid Fitri inayotarajiwa hivi karibuni.

Alisema maombi hayo yamekuja kufuatia maagizo aliyoyatoa Apirili 16 mwaka huu kwa taasisi zote za umma kuwapa mapema mshahara wa mwezi huu watumishi wa umma ili wafurahie vizuri sherehe za sikukuu, baada ya Mfungo mtukufu wa Ramadhan.

Rais Dk. Mwinyi alisema baada ya maagizo yake alipokea maombi mengi kutoka kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ili nao wafaidike lakini kwa vile hana mamlaka na sekta binafsi, aliziomba sekta hizo waridhie maombi yake na wawape mishahara wafanyakazi wao baina ya leo na kesho.

Akizungumza kwenye halfa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisifu juhudi za Rais Al hajj Dk. Mwinyi katika kuungamkono na kuendeleza masula ya khairati nchini.

Alisema tokea kunza kwa Mfungo mtukufu wa Ramadhan, Al hajj Dk. Mwinyi amefanikiwa kufutarisha nchi nzima kwa mikoa yote ya Unguja na Pemba, aidha, aleleza taifa limemshuhudia akishiriki ibada za sala za pamoja na wananchi wake zikiweo Ijumaa na Taraweikh kwa kipindi chote cha swaum kwa maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa huduma za kibenki kutoka Benki kuu ya watu wa Zanzibar (PBZ), Said Muhamed Said, alisema benki hiyo haiko nyuma kwenye kujikita na masuala ya jamii ili kuendelea kuwa karibu na wateja wake. Alisema PBZ inawajibu wa kushirikiana na Serikali kwenye kupata vijana wenye maadili mema pamoja na kuiunga mkono serikali kukuza na kuendeleza maadili ya vijana.

PBZ ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo waliiomba jamii kuendelea kuitumia ili na wao waendelee kuungamkono shughuli za jamii.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazi Zanzibar (ZBC), Salum Ramadhan Abdalla Shaaban ambao ni waratibu wa mashindano hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, alisema mashindano hayo yalianza mwaka jana baada ya kuzaliwa wazo na ZBC kabla ya kuliwasilisha Wizara ya Habari ambayo mafanikio yake yamekua endelevu hadi sasa.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji, Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, yaliibua washindi watatu, mshindi wa kwanza alizawadiwa gari aina ya Alphad, mshindi wa pili bodaboda na mshindi wa tatu fedha taslimu, shilingi milioni mbili.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

Post a Comment

0 Comments