Ticker

6/recent/ticker-posts

WATU 400 KUFANYIWA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO-MBALALI



Na. WAF-Mbalali

Zaidi ya watu 400 wenye matatizo ya macho kupatiwa matibabu ikiwemo ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika kambi ya siku 10 itakayaofanyika kwenye hospitali ya wilaya ya Mbalali.

Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa huduma za Macho kutoka Wizara ya Afya Dkt. Greater Mande amesema kuwa kambi hiyo inayoendeshwa na Wizara ya Afya kupitia watoa huduma kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda-Mbeya na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Mbeya kwa kushirikiana na Shirika la Hellen Keller International.

Amesema mradi huu wa upasuaji wa mtoto wa jicho utatekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja wilayani hapa na mpaka kumalizika kwa mradi huu, watu wapatao 900 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.

“Ulemavu wa kutokuona haukubaliki kwani zipo njia za kuzuia na kutibu zikiwemo za gharama nafuu, hivyo nawasihi wakazi wa Mbalali kujitokeza kwa wingi kwani huduma hizi tembezi zimewafikia na hazina gharama yeyote”.

Aidha, amesema Shirika hilo linatumia njia ya kuwaibua wagonjwa kwa kupita nyumba kwa nyumba kwa hatua ya awali na baadae kuwafikisha kwenye kituo cha kutolea huduma kwa ajili ya upasuaji.

Amesema dharima ya Serikali ya Awamu wa Sita kwa kushirikiana na wadau wa huduma za macho nchini kwa kufuata vipaumbele vya Wizara ya Afya ni kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na hasa wale ambao wapo mbali kwa kutumia huduma tembezi kwani Serikali imeboresha miundombinu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Naye, Meneja Mradi wa Shirika la Hellen Keller International Bw. Athuman Tawakal amesema kambi hiyo ni ya kwanza katika wilaya ya Mbalali na wanatarajia kuwafikia watu takriban 900 kutoka vitongoji vyote.

Tawakal ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu katika hospitali za Wilaya ikiwemo “theater “na hivyo kurahisisha huduma za upasuaji kufanyika kwenye wilaya.

Wakati huo huo Mkazi wa kijiji cha Muungano Bi. Victoria Mronji ambaye amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya mtoto wa jicho na kusababisha kutokuona kwa muda wa mwaka sasa ameishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma hizo karibu na bila gharama yeyote na kuahidi kuwa balozi mara baada ya kurudi kijijini kwao na kuwashauri watu wasisubiri hadi ugonjwa kuzidi hivyo kuwahi kufika kwenye kituo cha kutoa huduma za afya kupata matibabu.


Post a Comment

0 Comments