Ticker

6/recent/ticker-posts

ALAT WATAKIWA KUJIRIDHISHA NA KAMPUNI WANAZOZIPATIA ZABUNI

Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wametakiwa kujiridhisha na Kampuni wanazoingia nazo mikataba ya kutoa huduma katika maeneo yao ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 29 Mei, 2023 na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa alipokuwa akiwasilisha mada katika mkutano wa 37 wa ALAT unaofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC), Jijini Arusha.

Bw. Nyaisa ameeleza kuwa, bado kuna changamoto katika Tawala za Mikoa ya kuingia mikataba na taasisi ambazo hazitambuliki kisheria au ambazo hazijakidhi vigezo. Hali hii inasababisha upotevu mkubwa wa rasilimali za Taifa.

“Mnapotaka kuingia mikataba na Kampuni yeyote ni muhimu kujiridhisha kwa kujua kama Mzabuni huyo ni halali, kwa kuangalia kama anawasilisha mizania ya kila mwaka, wanahisa wake ni watu gani pamoja na anuani zao ili kujiridhisha”, ameeleza Bw. Nyaisa.

Ameongeza kuwa mara kadhaa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa halmashauri mbalimbali kuingia katika migogoro na wazabuni ambao kimsingi hawakutakiwa kuwapa zabuni kama wangepata taarifa zao kutoka BRELA.

Bw. Nyaisa ameeleza kuwa, Wakala imewekeza nguvu nyingi kutoa mafunzo kwa Maafisa Biashara nchi nzima ili kuwajengea uwezo kuhusu huduma zake.

“Wakala imekamilisha awamu ya kwanza ya mafunzo kwa Maafisa Biashara wa mikoa 26 ya Tanzania Bara kwa awamu ya kwanza. Utekelezaji wa awamu ya pili umeanza kwa Maafisa ambao hawakupata mafunzo katika awamu ya kwanza na mpaka sasa mikoa kumi (10) imefikiwa.

"Wito wangu kwenu ni kwamba muwatumie vizuri Maafisa hao ili kuchochea urasimishaji wa biashara na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uanzishwaji wa biashara nchini”, amefafanua Bw. Nyaisa.

BRELA inashiriki Mkutano huo wa siku tatu (3) kuanzia tarehe 29 hadi 31 Mei, 2023 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wake wa ellimu kwa umma.

Post a Comment

0 Comments