Ticker

6/recent/ticker-posts

BALOZI SHELUKINDO AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA MABALOZI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana na kuzungumza na mabalozi wa China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan kwa nyakati tofauti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao.

Mabalozi waliokutana na Balozi Shelukindo ni Balozi wa China, Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Kenya, Mhe. Isaac Njenga, Balozi wa Norway, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet, Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali.

Dkt. Shelukindo amekutana na mabalozi hao katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili na kuahidi kuongeza ushirikiano katika sekta za elimu, michezo, biashara na uwekezaji.

“Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na China, Kenya, Denmark, Italia na Sudan ambapo uhusiano huo umesaidia kuwa na misingi imara ya ushirikiano kwa maslahi mapana ya Taifa letu na nchi zao,” alisema Dkt. Shelukindo

“Vilevile nimepata fursa ya kukutana na Balozi wa Sudan na amenijulisha juu ya uwezekano wa mapigano yanayoendelea nchini humo kufikia mwisho kwa njia ya makubaliano. Na amenihakikishia kuwa wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini Sudan watapokelewa na kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika.

Amesema tarehe 11 Mei, 2023 pande zinazopigana nchini humo zilisaini mkataba wa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano,” alisema Dkt. Shelukindo

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Sudan nchini, Mhe. Mustafa Ali amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumalizika kwa mapigano yanayoendelea nchini humo kwa njia ya makubaliano ya amani.

“Naomba nikuhakikishie kuwa Serikali ya Sudan itawapokea wanafunzi waliokuwa wanasoma nchini kwetu na kupata fursa ya kuendelea na masomo yao baada ya mapigano kumalizika,” alisema Mhe. Mustafa Ali

Naye Balozi wa China nchini, Mhe. ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendeleza harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati.

Kwa nyakati tofauti mabalozi hao wameishukuru Tanzania kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiupata wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuahidi kuwa nchi zao zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwa maslahi ya pande zote.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akisalimiana na Balozi wa Kenya nchini, Mhe. Isaac Njenga katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Norway nchini, Mhe. Mette Norgaard Dissing-Spandet katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Balozi wa Italia, Mhe. Marco Lombard. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Shwahiba Mndeme pamoja na Afisa wa Idara hiyo, Bi. Kisa Mwaseba.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza na Kaimu Balozi wa Sudan, Mhe. Asim Mustafa Ali katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments