Ticker

6/recent/ticker-posts

JAFO ATOA MAELEKEZO MRADI WA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI KONDOA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameielekeza Halmashauri ya Kondoa mkoani Dodoma kumaliza miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ifikapo Julai 15, 2023.

Ametoa maelekezo hayo leo Mei 09, 2023 alipofanya ziara ya kukagua shughuli za Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) na kubaini kutokamilika kwa uchimbaji wa visima virefu vya maji safi wakati tayari Serikali ilishapeleka fedha.

Dkt. Jafo alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu miradi na kutoa fedha ili wataalamu wa halmashauri watekeleze miradi lakini wameonesha kusuasua na hivyo wananchi kukosa huduma ya maji.

Alisema suala mazingira ni mtambuka hivyo lengo la mradi ni kuwanufaisha wananchi ili waweze kufanya shughuli mbadala za kiuchumi na kuachana na shughuli zinaazohusiana na uharibifu wa mazingira.

“Mkurugenzi nakutegemea kusimamia wataalamu wako wa halmashauri na RUWASA Kondoa ili uchimbaji wa visima ukamilike kwa wakati wananchi wamechoka kusubiri toka mwezi Oktoba mpaka leo mnasuasua wakati Serikali tayari ilishawaletea fedha,“ alisema.

Alisema suala la mazingira ni mtambuka na ndio maana Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu miradi inayohusisha ufugaji, kilimo, maji na ardhi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hivyo lazima kulinda mazingira na ndiyo maana Serikali ikapeleka mradi huu kwa wananchi wa halmashauri hiyo ili wapate shughuli mbadala za kiuchumi za kufanya pamoja na kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika hatua nyingine amekagua shamba darasa la ng’ombe wa maziwa la kikundi cha UHAI katika Kijiji cha Mafai pamoja na ujenzi wa eneo la ukusanyaji maziwa, kisima, kikundi cha shamba la mfano la ufugaji nyuki pamoja na kilimo hifadhi cha zao la mahindi kwa kutumia teknolojia.

Katika miradi hiyo, Dkt. Jafo amewapongeza kwa utekelezaji na kusema ameridhishwa kwani pamoja na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inayoathiri kilimo mradi huo unasaidia wakulima kupata tija.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Dkt. Khamis Mkanachi alisema miradi hiyo imeleta manufaa makubwa kwa wananchi wilayani humo hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema miradi hiyo hususan wa ng’ombe utaongeza thamani ya mifugo ambapo kupitia kilimo cha mahindi cha teknolojia ya kisasa inawasaidia wananchi kupata mazao na hivyo kukuza uchumi wao.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za mradi na hivyo nakuahidi changamoto hizi ulizozikuta hapa tutazifanyia kazi,“ alisema.

Mradi wa LDFS unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) unatekelezwa pia katika Halmashauri zingine ikiwemi Nzega (Tabora), Magu (Mwanza), Kondoa (Dodoma) na Micheweni (Kaskazini, Pemba).


Post a Comment

0 Comments