Ticker

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU DKT. YONAZI: ELIMU ZAIDI ITOLEWE KUPINGA UNYANYAPAA KWA WAVIU

NA. MWANDISHI WETU

Imeelezwa kuwa elimu inapaswa kuendelea kutolewa katika jamii kupinga vitendo vya unyanyapaa kwa Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini ili kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya UKIMWI katika Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi mapema Mei 9, 2023 alipokutana na uongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini (NACOPHA).

Akieleza jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI, Dkt. Yonazi amesema ipo mikakakti madhubuti ya kuendelea kuelimisha umma kuhusu kupinga masuala ya unyanyapaa kwa WAVIU huku akiiasa jamii kuwa mstari wa mbele katika jitihada hizo.

“Afua mbalimbali za masuala ya UKIMWI zimeendelea kuonesha jitihada za Serikali katika mapambano haya, nitoe rai elimu iendelee kupewa kipaumbele ili kupinga unyanyapaa kwa WAVIU,”alisema Dkt. Yonazi.

Dkt Yonazi aliongezea kuwa, ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa NACOPHA ili kuhakikisha sifuri tatu zinafikiwa ifikapo 2030.

“Tutaendelea kushirikisha wadau mbalimbali lengo kuhakikisha tunayafikia malengo, na ofisi yangu ipo tayari kutoa ushirikiano wakati wote kuhakikisha masuala yote ya uratibu yanatekelezwa vizuri ili kuendelea kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuhakikisha tunaondoa unyanyapaa katika jamii,”alisisitiza

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa NACOPHA Bw.Deogratius Rutatwa alipongeza jitihada za Serikali kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kurahisisha utendaji wa Baraza hilo.

“Hadi sasa tuna jumla ya wanachama laki sita na elfu sabini na mbili pamoja na vikundi vya WAVIU 3769 katika shughuli za kujipatia maendeleo yao ambavyo vinatoa fursa kushiriki katika shughuli mbalimbali na tunatumia kuhamasisha watu kuendelea kupima virusi vya UKIMWI na utumiaji wa dawa kwa wanaogundulika na maambukizi,”alisema Deogratius.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu) Dkt. Jim Yonazi akipokea nyaraka kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bw.Deogratius Rutatwa mara baada ya mazungumzo yao ya kikazi Mei 9, 2023 Jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bw.Deogratius Rutatwa akieleza majukumu ya ofisi yake kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu) Dkt. Jim Yonazi walipomtembelea ofisini kwake Mei 9, 2023 Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza na timu ya watendaji kutoka NACOPHA (hawapo pichani) wakati wa kikao chake na ujumbe huo, walipomtembelea ofisi kwake Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu) Dkt. Jim Yonazi akioneshwa nyaraka na Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bw.Deogratius Rutatwa walipomtembelea na kufanya mazungumzo katika Ofisi yake Jijini Dodoma.
Mratibu wa Dawati la masuala ya UKIMWI Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Adela Mpina akizungumza jambo wakati wa kikao cha ujumbe kutoka NACOPHA.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaribu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), mara baada ya mazungumzo yao Mei 9, 2023 Dodoma.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Post a Comment

0 Comments