Ticker

6/recent/ticker-posts

RTO MKOANI TANGA AWAFUNDA MADEREVA NA MAKONDAKTA, VIBAKA MARUFUKU STENDI.

Kamanda wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga Willy Mwamasika akiongea na madereva pamoja na makondakta katika stendi kubwa ya mabasi yaendayo Mikoani iliyopo Kange jijini Tanga.

************************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

KAMANDA wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga Willy Mwamasika amesema madereva wana mchango mkubwa katika kuimarisha na kukuza uchumi hivyo wana wajibu mkubwa wa kufanya kazi zao kwa weledi ili kuepusha madhara kwa wananchi.

Mwamasika ameyasema hayo wakati akiongea na madereva pamoja na makondakta katika stendi kubwa ya mabasi yaendayo Mikoani iliyopo Kange jijini Tanga kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wao wakiwa kazini.

"Kila mtu ana nafasi yake katika uchangiaji wa uchumi, kwahiyo na ninyi hii kazi mnayoifanya mna mchango wenu katika ukuaji wa uchumi wa Tanga, ilimradi tu katika utekelezaji wenu mhakikishe hamvunji sheria, kwasababu mnabeba abiria kuwawahisha katika majukumu yao ya kuchangia uchumi,

"Hivyo basi mna wajibu wa kuchukua tahadhari zote mnapokuwa barabarani ili kuhakikisha hamleti madhara kwa abiria wenu, madereva wana wajibu wa kuhakikisha wanaendesha kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Usafirishaji" amesema.

Aidha Mwamasika amewataka madereva hao kufanya kazi kwa weledi ili kuepuka kusumbuana na askari wa barabarani kwani itasaidia kila mmoja kuwa na uhuru anapokuwa katika eneo lake la kazi.

Mwamasika pia amepiga marufuku kwa maajenti wanaotafuta abiria kuwafanyia usumbufu kwa kuwavuta na kusababisha kero kwa abiria hao, ikiwa ni pamoja na vibaka wanaokwenda stendi kwa ajili ya kutekeleza wajibu wao wa kuibia watu.

"Ni matumaini yangu mmenielewa na mtatekeleza majukumu yenu ipasavyo, nite onyo kwa wale wenzetu ambao wanakuja stendi kwa ajili ya kufanya wizi wa kuibia wasafiri, stendi yetu ni nzuri na haina dosari hivyo watu hawa ni marufuku kuingia hapa, hawana nafasi kwqni hawa ndio wanaotuharibia" amesema.

"Na ninyi mnaofanya kazi zenu za kutafuta abiria hapa mtoe taarifa kuwafichua hawa vibaka ili tuwaondoe watuachie stendi yetu, nina imagine mtafanya hivyo ili tunapokutana barabarani tuwe tunapungiana na sio kufuatana mwisho wa siku tunachukiana" ameongeza.

Hata hivyo Mwamasika amewaasa madereva wanaendesha mwendo wa kasi kufuata maelekezo ya serikali kwa kutembea mwendo wa kawaida uliopangwa kwakuwa atakayekiuka mbali na adhabu lakini pia ipo adhabu kubwa ya kufutiwa leseni aliyonayo ili akaanze upya kuipata.

"Nadhani mmenielewa madereva, tembeeni mwendo wa serikali, sasa hivi dunia ni kama kijiji, usije ukasema hatukuoni huko barabarani, ulipo na sisi tupo, kwa atakayekiuka agizo hilo atapigwa faini na atakapoendelea atalazimika kufungiwa leseni, na atakapofungiwa atalazimika kuanza upya kuomba, lakini pia tutakuangalia kama utakuwa na vigezo, usipotimiza uachane na udereva unde ukatafute kazi za kufanya" amesema.

Vilevile ametoa wito kwa madereva wote wa mabasi makubwa na daladala kuanzia wenye madaraja class C na E, kwamba zoezi la uhakiki wa leseni hizo wa hiyari bado linaendelea, na baada ya muda ukifika serikali itaanza msako wa kukamata madereva ambao hawajahakiki leseni zao.

"Sasa hivi njoo na leseni yako tukuhakiki kama ni halali tutakupa barua ya kutembea nayo kwamba wewe umehakikiwa na upo kihalali, lakini suala la upatikanaji wa leseni ni lazima ukasome, nendeni kwenye vyuo vinavyotambulika kisheria, baada ya hapo ulete barua ya maombi na utapatiwa keseni kulingana na madaraja ya chuo ulichosomea" amebainisha.

Post a Comment

0 Comments