Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI: WANANCHI MSIJENGE MABONDENI KUEPUKA MAFURIKO

Serikali imewataka wananchi waache kujenga katika mabondeni kwakuwa maeneo hayo ni rahisi kutuama maji hivyo kusababisha mafuriko ambayo huathiri Maisha yao.

Hayo yamesemwa bungeni leo Mei 08, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohamed Haji.

Katika swali lake la msingi Mhe. Zahor alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kudhibiti mafuriko ambayo husababisha uchafuzi wa mazingira na kuongeza umaskini katika Jimbo la Mwera.

Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema inahitajika pia elimu itolewe kupitia halmashauri zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar kuhusu umuhimu wa kujenga nyumba maeneo yaliyopimwa kwani kwani tayari yamekidhi vigezo vya kutumika kwa makazi.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kufanya tathmini ya kina katika maeneo yote yanayokumbwa na mafuriko nchini katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Alifafanua kuwa tayari Serikali imechukua hatua za kuunda Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ yenye jukumu kuu la kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Wilaya wa Kukabiliana na Maafa ya mwaka 2022.

Naibu Waziri Khamis aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na hatua za kuunda kamati hiyo pia Serikali imeendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na maafa yakiwemo mafuriko.

Post a Comment

0 Comments