Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKALA WA VIPIMO MKOA WA KIGOMA YAHIMIZWA KUENDELEA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KWENYE MAWESE

Kufuatia ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) aliyofanya Mkoa wa Kigoma akiwa na lengo la kuhamasisha kilimo cha mchikichi ambapo katika ziara hiyo aliagiza kutokomezwa kwa vipimo batili maarufu kama bidoo kwenye biashara ya mawese kwa kuwa vinawapunja wakulima wa zao hilo.

Katika utekelezaji wa agizo hilo wakala wa vipimo imefanya kikao na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma ambapo katika ufunguzi wa kikao hicho akizungumza mgeni rasmi Mhe. Kanali Michael Ngayalina Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema ni ukweli usiopingika kwamba matumizi ya vipimo na udhibiti wake, hususani kwenye biashara ya mawese umekuwa na changamoto nyingi.

Baadhi ya changamoto hizo ni kukosekana kwa masoko/vituo rasmi vya kufanyia biashara ya mawese kwenye maeneo mengi, hali inayotoa mwanga kwa wanunuzi kununua mawese kwenye vinu vya uzalishaji na wakati mwingine kwenye nyumba za wananchi (wakulima) wetu. Hali hii siyo tu kwamba inafanya kazi ya udhibiti wa matumizi ya vipimo kuwa ngumu, bali huikosesha serikali (mamlaka zetu) sehemu ya ushuru pamoja na kushindwa kupata takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo ya mawese.

Kadhalika, Mgeni rasmi Kanali Michael Ngayalina ameipongeza taasisi ya Wakala wa Vipimo kwa kuendelea kusimamia matumizi ya vipimo kwenye maeneo mbalimbali ya biashara na huduma pamoja hatua walizokwisha chukuwa kufikia sasa kudhibiti matumizi ya BIDOO kwenye biashara ya mawese kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa wetu ili kuhakikisha biashara hiyo inafanyika kwa haki na usawa bila upande wowote kupunjika na ameitaka Wakala wa Vipimo kusaidia upatikanaji wa vibaba vya gharama nafuu ambavyo vitatumika kupimiwa mafuta ya mawese.

Akizingumza wakati wa kikao Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Kigoma Bw. Laurent Kabikiye ameeleza kuwa wakala wa Vipimo inatoa elimu mara kwa mara kuhusiana na madhara ya kutumia vipimo batili (Bidoo) ili kuweza kumlinda mkulima wa zao la chikichi na mnunuzi pia. Pamoja na elimu hiyo wakala wa vipimo inafanya jitihada za kutafuta vipimo vitakavyo patikana kwa gharama nafuu (Kibaba) ambavyo vitakuwa na ujazo mbalimbali ili kuwasaidia wafanyabiashara wa mawese kuweza kuuza bidhaa zao kwa kutumia kipimo hicho ambacho ni sahihi ili kuwasaidia kupata faida bila kupunjwa.

Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma kama Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma, Makatibu Tawala wasaidizi sekretariet ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Mkoa, Maafisa Tarafa, Maafisa Biashara kutoka Halmashauri zote za Mkoa, Meneja wa SIDO na TBS pamoja na watumishi wa Wakala wa Vipimo.

Aidha, washiriki wa kikao kazi hicho kwa pamoja wamekubaliana kuwa Halmashauri zianzishe masoko (Buying Centres) za kuuzia na kununulia mawese pamoja na kununua vipimo vilivyohakikiwa na Wakala wa Vipimo na kuhamasisha wauzaji wa mawese kununua vipimo ili vitumike kununua na kuuzia mawese na kutokomeza matumizi ya vipimo batili (Bidoo).


Post a Comment

0 Comments