Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KULINGANA na takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Tanga umekuwa na ongezeko la watu kutoka milioni 2,470,205 mwaka 2012 hadi kufikia milioni 2,615,597 mwaka 2022 ukiwa na ongezeko la watu 145392.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba ametoa takwimu hiyo wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa Sekretarieti ya Mkoa, Kamati ya sensa ya Mkoa pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ambapo alisema hatua hiyo inaonesha ni kiasi gani mahitaji yameongezeka.
“Pamoja na kwamba kiwango hiki ni kidogo, ni muhimu kutafakari chanzo cha ongezeko hili na namna ya kupata kipato, kwahiyo ni wajibu wetu kupanga mipango madhubuti ya maendeleo ikiwemo huduma ya miradi mbalimbali, pamoja na matumizi bora ya ardhi ikiwemo mipango ya miji na maeneo ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya wananchi" amesema
Aidha Kindamba amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya matokeo ya sensa nna kusema, “yanatuwezesha kufanya maamuzi yenye kufuata vigezo vya takwimu badala ya mtu binafsi, serikali ya awamu ya sita inataka kuona rasilimali za nchi zinagawanywa kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya watu, mahitaji yao na mazingira wanayoishi
“Si vema kuona rasilimali za nchi zimerundikana sehemu moja, iwe Kata, Wilaya au Mkoa wakati kuna Mikoa mingine kuna uhitaji, haiwezekani, kwa maana nyingine matokeo ya sensa mwaka 2022 na takwimu nyingine zinazozalishwa ziwe zinakwenda kwenye dira ya kuongoza katika kufanya maamuzi”
Kindamba amesema katika bajeti ya mwaka 2023/24 Mkoa wa Tanga umezingatia matokeo ya sense ya mwaka 2022, hivyo dira inawaongoza na kwamba umezingatia sensa ya anuani za makazi.
Akitoa maelezo mafupi kwa niaba ya Mtakwimu mkuu wa serikali Tonny Mwanyoti ambaye ni Mratibu wa sensa MKoa wa Tanga amesema bado matokeo ya sensa ya watu na makazi yanaendelea kutolewa ambapo mapema mwezi februari mwaka, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua ripoti tatu za mgawanyo wa idadi ya watu kwa maeneo au utawala, umri na jinsia pamoja na majimbo ya uchaguzi.
Mafunzo haya yanayoendeshwa na Ofisi ya Taifa wa takwimu na Mtakwimu mkuu wa serikali ya Zanzibar yanafanyika kwa mujibi wa mpango kazi na usambazaji huu na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022 na yanashirikisha makundi mbalimbali katika jamii yetu, ameeleza
"Mpaka sasa mafunzo haya yamefanyika kwa makundi ya viongozi wa ngazi za chini katika Mikoa ya Dar as salaam, Dodoma, Kigoma, Morogoro, Linda na Mikoa mitano ya Zanzibar, lakini pia yametolewa kwa wahariri vyombo vya habari zaidi ya120 nchini" amesema Mwanyoti.
Hata hivyo amebainisha kwamba utekelezaji wa mpango kazi wa usambazaji wa mafunzo ya matokeo ya sensa, chimbuko lake ni muongozo wa Kitaifa ambao umeelekeza mafunzo haya yatolewe kuanzia ngazi ya Taifa hadi chini kwa makundi mbalimbali kama ilivyokuwa wakati wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika sensa ya watu na makazi".
"Kwamaana hiyo, mpango kazi huo unatuelekeza kurudi kwenye makundi yote katika jamii ambayo yalihusishwa wakati wa maandalizi, hususani uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi mwaka 2022, hivyo napenda kuwahakikishia washiriki na wadau wote nchini kwamba mafunzo haya, yatafanyika kama mpango kazi ulivyoelekeza" amebainisha.
Baadhi ya viongozi wa kamati ya Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Kamati ya Sensa MKoa wakifuatilia mkutano.
0 Comments