Ticker

6/recent/ticker-posts

SITAKI TENA KUSIKIA MGOGORO HUU, NIMESHAUMALIZA, ANAYEJIONA KIDUME ATAKUTANA NA JWTZ

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba akiongea na wananchi wa vijiji vya Gitu na Ngobole.
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa Mkoa.

**************

Na Hamida Kamchalla, KILINDI.


KUFUATIA agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya vijiji vya Gitu na Ngobole wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga, jana (1/9), mgogoro huo umemalizwa huku maagizo kadhaa yakitolewa kwa viongozi wilayani humo.


Akiwa katika kjiji cha Gitu, Kindamba ameongea na wananchi wa vijiji hivyo ambapo alimaliza mgogoro huo na kusema kuanzia siku hiyo hataki kusikia mgogoro wowote ukiendelea na atakayejaribu hatavumiliwa kwani eneo linalogombaniwa litakuwa chini ya Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ).


Amesema mgogoro huo unahusisha vitongoji viwili vya Komtindi na Ngaloji ambao umedumu kwa miaka 17 ukiwa na utata wa kila kijiji kudai vitongoji hivyo viko upande wake lakini uhalisia vinapata huduma zote za kijamii kutoka kijiji cha Gitu na pia ramani inaonesha hivyo.


"Hakuna mwenye mamlaka ya kumiliki ardhi ila Rais wa nchi hii, na huku sisi watumishi wake ndio tuna mamlaka kwahiyo kuanzia leo natangaza kwamba vitongoji hivi viwili ni vya kijiji cha Gitu, halfu cha kushangaza ni kwamba tangu enzi na enzi vitongoji hivi vinaitika Gitu,


"Huduma zote za kijamii wanazipata Gitu, kura na sensa vyote wamefanyia huko, kwanini Ngaloji isema ni vyao, haiwezekani" amesema na kuhoji Kindamba.


Aidha Kindamba amewaasa wananchi kwamba suala la kupambana na kusuhisha migogoro siyo kipaumbele chake bali ni kuhakikisha anawaletea maendeleo hususani barabara ambazo zitaunganisha mawasiliano na kufungua uchumi wa Mkoa na kwa faida ya Taifa.


"Tusiumizane kichwa mimi nina mambo mengi ya kufanya hasa katika kuwaletea wananchi wa Tanga maendeleo, sisi tunatakiwa kuangalia mbele kila mmoja kwa nafasi yake na kupambana kujua hii barabara ya Handeni - Kilindi - Kiberashi hadi Kiteto,


"Tuimbe hivyo kwasababu hii barabara itakapokamilika watakaokuwa wanataka kwenda bandari ya Dar es salaam wasiende huko, waje bandari Tanga, barabara iwe inafanya kazi muda wote, watu walime na biashara ziende kwenye masoko" amesema.


"Sisi tuna ardhi yenye rutuba, lakini kwasababu akili yetu tunaishuhulisha kwenye migogoro, acheni na baada ya kikao cha leo tutashuhulika nae sisi kama serikali, hatutaki kusikia mgogoro huu tena" amesisitiza.


"Kati ya Gitu na Ngobole, katikati kuna msitu upo pale, eneo lile tunawakabidhi Jeshi la Wananchi (JWTZ) na tangu awali walishaliomba lakini serikali haikuwapatia, kwahiyo mkiwaona wanazunguuka pale, wapo kwenye maeneo yao wanafanya mazoezi" amesema.


Amebainisha kwamba kwa kufanya hivyo, mbali ya kwamba watakuwa wakifanya mazoezi lakini pia watakuwa wanaimarisha hali ya ulinzi na usalama hivyo wananchi wanapaswa kujua na kulipokea.


Kindamba ameagiza serikali za vijiji hivyo kukaa na kutengeneza mihutasari kuhusu maamuzi aliyotoa kwenye kikao hicho ambapo alimsisitiza mkuu wa Wilaya hiyo Hashimu Mgandilwa kuwasimamia wenyeviti hao.


Lakini pia amewataka Mkurugenzi na Mwenyekiti wa halmashauri kuweka vizingiti vya kutenganisha maeneo hayo ili kila mmoja awesome kwenye eneo lake stahiki.


Hata hivyo amewataka wenyeviti wa vijiji kuacha tabia ya kuuza ardhi bila kufuata taratibu kwani mihuri wanayotumia ilishapigwa marufuku hivyo atakayefanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake bila kuonewa huruma.


"Nasikia mna mihuri, hiyo ilishapigwa marufuku, ukiuza eneo na ukapiga muhuri hilo ni kosa, utakuwa umegushi, na tutashuhulika na wewe kwa mujibu wa sheria za nchi za kugushi na hatutakutazama usoni hata uwe nani" amesisitiza.


"Nataka nikitoka hapa niende nikaandike ripoti kwa Mh. Rais kwamba mgogoro huu nimeutatua na sasa hali ni shwari, wananchi wanaendelea na shuhuli zao, hivyo niombe mambo yatakayoleta maendeleo katika Wilaya hii na siyo nikaombe kusaidiwa kutatua mgogoro" ameongeza.

Post a Comment

0 Comments