Ticker

6/recent/ticker-posts

PROFESA MUKANDALA AELEZA SABABU ZA KUZAMA KWA MV. BUKOBA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala amesema kuzama kwa Mv. Bukoba kulitokana na sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni meli kukosa ustahimilivu na kulala upande mmoja na kisha kuzama.

Ameyasema hayo Mei 21, 2024 katika mhadhara wa uprofesa uliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete, viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa elimu nchini.

Amesema sababu zingine ilikuwa ni uchache wa maji kwenye baadhi ya matenki, wingi wa abiria zaidi ya kiwango ambacho meli ilipaswa kubeba, na wingi wa mizigo.

Aidha amesema kuwa Sababu nyingine ilikuwa uzembe wa wafanyakazi wa meli na taasisi husika kushindwa kusimamia vizuri uendeshaji wa meli.

Hata hivyo amesema kuwa meli ya MV. Bukoba haikuwa na hali nzuri ya kusafiri kwani ilionesha dalili za kukosa ustahimilivu mapema.

“Tume ya Jaji Kisanga inasema kwamba, wingi wa abiria uliopitiliza, wingi wa mizigo ikiwemo iliyowekwa katika deki, na kiwango kidogo cha maji kwenye matenki ilisababisha chombo kusafiri kutoka ghuba ya Kemondo kwa namna ya hatari, hakikuwa na uimara wowote kwa sababu hiyo tume inaona wakati wa safari MV Bukoba haikuwa katika wakati mzuri wa kufanya safari kwa maana nyingine haikupaswa kuwa majini.

“Ilikuwa vigumu kwa meli kuondoka Kemondo na baadhi ya wanusurika wanasema ilikuwa ikilalia upande moja kitu ambacho kilianza kuenekana baada ya meli hiyo kuondoka Bukoba, ikiwa safarini meli hiyo ilikuwa ikiserereka polepole kila baada ya muda Fulani na maji yalikuwa yakiingia ndani ya meli,” amesema Profesa Mukandala

Pamoja na hayo ameeleza kuwa baada ya meli kuzama inasemekana kuwa, baadhi ya abiria walikufa baada ya kupigwa shoti na jenereta lililokuwa linaendelea kufua umeme katika meli hiyo, pia baadhi ya watu yawezekana walikunywa mafuta na kuwafanya washindwe kupumua.

Vilevile ameeleza kuwa tume hiyo ilibaini kuwa mashua ya kuokoa iliyokuwa chini ya Kamanda wa Polisi haikuwa na mafuta, mawasiliano kati ya Dar es salaam na Mwanza yalifanywa kwa polepole, Jeshi la Maji la Tanzania halikuwa hata na mpiga mbizi moja.

Post a Comment

0 Comments