Ticker

6/recent/ticker-posts

BRELA YAWAKUMBUSHA WAFANYABIASHARA KUSAJILI BIASHARA ZAO


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAFANYABIASHARA Mkoa wa Tanga wamekumbushwa kusajili au kuhuisha kampuni au biashara zao kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) badala ya kusubiria kupata tatizo pindi wanapotaka huduma zinazohitaji leseni.


Ofisa Sheria BRELA, Lupakisyo Mwambinga ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 11 ya Biashara mkoani humo huku akigusia kuhusu upatikanaji wa zabuni mbalimbali zinazotolewa ambapo wafanyabiashara watatakiwa kufanya maombi ili kuzifanikisha.


Amesema BRELA ipo kwa ajili ya kusajili biashara hivyo inawapasa wenye uhitaji kuwafikia na kupata maelekezo ya kina kwakuwa huduma hiyo sasa inapatikana Kwa njia ya kidigitali.


"Mara nyingi tunapenda kuwapa elimu wafanyabiashara umuhimu wa kusajili au kuhuisha, kwasababu wengi wanasubiri labda wamepata uzabuni na kutaka cheti kutoka BRELA ndio wanakuja kusajili,


"Kwahiyo sasa hivi kila mahali wanahitaji cheti cha usajili kutoka BRELA, kwahiyo nawashauri watu wasajili biashara zao lakini pia kupata leseni inayostahili,


"Watu wengi wanachanganya hizi leseni daraja A na daraja B ambazo zinatolewa na halmashauri na manispaa, hizi ni tofauti, kuna biashara ambazo zina sura ya Kitaifa na Kimataifa unatakiwa uwe na leseni ya BRELA" amesema.


Hata hivyo amefafanua kwamba wale wajasiriamali na wenye viwanda vidogo vidogo wanapatiwa leseni za viwanda, "watu wengi hawajui kwamba unapofungua kiwanda ni lazima uwe na leseni, kwahiyo kuna leseni ya kiwanda na biashara".

Post a Comment

0 Comments