Ticker

6/recent/ticker-posts

MSHOMBA AFICHUA SIRI MAFANIKIO YA NSSF

*Asema mazingira mazuri ya uwekezaji chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia yamechochea mafanikio

Na MWANDISHI WETU

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba amefichua siri ya mafanikio makubwa ambayo NSSF imeyapata kuwa yamechangiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyohamasisha wawekezaji katika sekta binafsi, kuweka mazingira mazuri na kuwezesha kupata waajiri na wanachama wengi wapya katika sekta binafsi.

Bw. Mshomba amesema hayo tarehe 3 Julai, 2024 wakati alipotembelea banda la NSSF mara baada ya ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu SabaSaba yaliyobeba kauli mbiu isemayo "Tanzania Sehemu Sahihi kwa Biashara na Uwekezaji." Maonesho hayo yamefunguliwa na Mhe. Filipe Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji akisindikizwa na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda hilo la NSSF, Bw. Mshomba amesema kwa mujibu wa taarifa za hesabu ambazo hazijakaguliwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, thamani ya NSSF kwa sasa inafikia trilioni 8.5 sawa na ongezeko la asilimia 77% ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita.

“Ongezeko hili ni kubwa hasa ukizingatia kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita ukuaji wa NSSF umekuwa mkubwa mno,  hivyo tunampongeza sana Mhe. Rais Dkt. Samia kwa juhudi anazoweka katika kuhakikisha mazingira ya biashara hapa nchini yanakuwa mazuri ambayo yamechangia mafanikio haya,” amesema Bw. Mshomba.

Amesema wakati NSSF inaendelea kutekeleza mpango wake wa maendeleo unaoishia Juni 30, 2026, wanatarajia thamani ya Mfuko kufikia trilioni 11 ambayo itakuwa ni zaidi ya mara mbili ukilinganisha na kipindi ambacho Rais Dkt. Samia alipoingia madarakani.

Bw. Mshomba amesema kwa sasa NSSF imeelekeza nguvu ya kuwafikia wanachama wapya waliopo katika sekta isiyo rasmi ili waweze kujiunga na kuchangia katika NSSF kwani tayari wameshaweka mifumo mizuri ya usajili na uchangiaji pamoja na mafao yanayovutia kupitia Mpango wa Kitaifa wa Sekta Isiyo Rasmi.

Amesema ushiriki wa NSSF katika maonesho hayo ni kwa ajili ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachama na wadau kuhusu huduma mbalimbali ambazo NSSF unazitoa zikiwemo usajili wanachama kutoka sekta binafsi na sekra isiyo rasmi, uchangiaji, kulipa mafao, uwekezaji pamoja na uhakiki wa wastaafu.

Bw. Mshomba amesema pia wanatumia maonesho hayo kuwaeleza wanachama mambo makubwa ambayo NSSF imeyafanya kupitia huduma za TEHAMA ambapo sasa wanachama wanaweza kujisajili kupitia lango la huduma binafsi kwa mwanachama (Member Portal) na lango binafsi kwa mwajiri (Employer Portal).

Amesema NSSF inaendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini hivyo wataendelea kuboresha huduma zao mbalimbali. 

Post a Comment

0 Comments