Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa elimu kwa wafanyabiashara wa mazao ya misitu katika eneo la Mbezi Kwa Msuguli, jijini Dar es Salaam, kuhusu sheria na taratibu zinazopaswa kuzingatiwa katika shughuli hizo.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo leo, Agosti 26, 2026, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS Kinondoni, Dennis Mhagama, amesema lengo ni kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa taratibu za uvunaji, usafirishaji, umiliki na usajili wa mazao ya misitu ili waendeshe shughuli zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Mhagama amesema uelewa wa taratibu hizo ni muhimu katika kuzuia ukiukwaji wa sheria na kuhakikisha biashara ya mazao ya misitu inafanyika kwa njia halali na endelevu.
“Tumewafundisha namna ya kufuata taratibu za uvunaji, usafirishaji na umiliki wa mazao ya misitu, pamoja na taratibu za usajili, ili waweze kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria,” amesema.
Aidha, amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanapata mkaa kutoka kwa wazalishaji wenye vibali halali, hatua itakayosaidia kupunguza ukiukwaji wa sheria za misitu.
Kwa upande wake, Nevitory Mushi, mfanyabiashara wa mkaa katika eneo la Kwa Msuguli, Mbezi, ameishukuru TFS kwa kuwafikia na kuwapatia elimu hiyo, akisema imewaongezea uelewa kuhusu sheria na taratibu za biashara ya mazao ya misitu.
Naye Samweli Ndomba, mfanyabiashara wa mkaa, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu taratibu za usajili na namna ya kuendesha biashara hiyo kwa kuzingatia sheria.
Amesema awali baadhi yao hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu zinazotakiwa, lakini elimu iliyotolewa imewasaidia kufahamu hatua sahihi za kufuata katika shughuli zao.













0 Comments