-Majiko 3,126 kusambazwa wilaya zote 3 za Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko ametoa wito kwa wananchi wa Katavi kuchangamkia fursa ya kununua majiko banifu kwa bei ruzuku ya shilingi 7,500 yanayosambazwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kulinda afya, kuokoa misitu na kuhifadhi mazingira.
Ametoa rai hiyo Desemba 18, 2025 Mkoani Katavi wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza majiko banifu ya ruzuku yapatayo 3,126 mkoani humo unaotekelezwa na Kampuni ya Tango Energy Ltd ya Jijini Dar es Salaam unaoratibiwa na kusimamiwa na REA wenye thamani ya shilingi milioni 156.3 ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034).
“Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi, majiko haya ni kwa ajili yenu na yameuzwa kwa bei ya ruzuku kwa maana ya kwamba Serikali imelipia zaidi ya shilingi 50,000 lakini mwananchi analipia shilingi 7,500 pekee, naomba mchangamkie fursa hii,” amesisitiza Mhe, Mrindoko.
Mhe. Mrindoko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amejielekeza katika kuhakikisha kwamba wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia.
Akitambulisha mradi, Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali alisema majiko hayo yatauzwa kwa shilingi 7,500 badala ya shilingi 59,000 kwakuwa Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya 85% sambamba na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika majiko hayo ili kumpa unafuu mwananchi.













0 Comments